KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Van Pluijm amesema wachezaji wengi wa Tanzania hawako tayari kucheza soka la kulipwa barani Ulaya na nchi nyingine zilizopiga hatua katika mchezo wa soka.
“Kwanza sijui kuhusu kutakiwa kwa wachezaji wangu kwenye nchi za Ulaya. Pili kila mmoja anapaswa kujiuliza kama wako tayari kwa ajili ya soka la kulipwa. Wote tunapenda kuona wachezaji wetu wakifanikiwa,” alisema Pluijm.Pluijm alisema kwamba kama kuna kitu cha kubadilisha kwenye soka la Tanzania ni mtazamo wa wachezaji na viongozi kuelekea kwenye soka la kulipwa, kwani mtazamo huo unamuandaa mchezaji kuwa tayari na soka la kulipwa.
“Kwa baadhi ya wachezaji ni kama utamaduni wa kushangaza kubadili akili na mtazamo wao. Lakini kama unataka kubadili kitu fulani kwa ujumla kwenye soka la Tanzania basi ni mtazamo wao kuelekea kwenye soka la kulipwa… “Kubadili mtazamo wao na kuwafanya wawe na shauku ya kutaka kupata tuzo binafsi, kwa klabu zao na timu ya taifa,” alisema Pluijm.
Kocha huyo kutoka Uholanzi na aliyeiongoza Yanga kufika hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka la Afrika, alisema kuwa wachezaji wa Tanzania wanatakiwa kuiga mfano wa mshambuliaji Mbwana Samatta ambaye kwa sasa anacheza KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji.
“Juma Mahadhi (mchezaji mpya wa timu hiyo kutoka Coastal Union) ana kipaji cha kumfanya acheze soka la kulipwa siku za usoni, lakini tunapaswa kuwa waangalifu na tunavyomchukulia asilewe sifa. Bado kijana mdogo anayetakiwa kujifunza mambo mengi kwenye mchezo wa soka,” alisema Pluijm.
No comments:
Post a Comment