Kulikuwa na Ronaldinho mmoja tu katika ulimwengu huu. Akaja Xavi na zile pasi zake nae ameenda zake. Juninho yule mchawi wa mipira iliyokufa nae ameenda na ufundi wake. Kuna wakati nilitamani sana kuwahi kuwaona Romario, Michel Platini na wenzao katika kizazi chao. Uchelewaji wangu nimeshindwa kupata vitu vingi vilivyo ndani yao.
Macho yananituma kuamini na kushukuru kwa hiki nachoendelea kukiona kutoka kwa Ronaldo na Messi katika kizazi chao.
Inaweza kuchukua miaka mingi ijayo kuona tena vitu wanavyofanya ndani ya uwanja. Dimitri Payet huyu naye anakuja katika mioyo yetu huku macho yetu yakiwa na mengi ya kujiuliza.
Kile anachoendelea kukifanya pale kwao Ufaransa ni mwendelezo wa miguu yake yenye thamani ya Buggati au ndiyo utakuwa mwisho wake wa kuipisha miguu yake ianze kusinyaa, ngoja nisubiri huku nikiendelea kuuangalia ukurasa wake kwa hiki anachoendelea kukifanya kule kwao Ufaransa.
Wakati mwingine natamani kuwahi kujua ubora wa macho yangu kwa vitu vingi ninavyoviamini. Niliwahi kusema hapo nyuma safari ya mshindi wakati mwingine huwa na mizunguko mingi mpaka kufika katika safari ya mafanikio. Kuna wanadamu wanaamini katika hili. Dimitri Payet niliwahi sema ubora wako naona bado unaendeleza thamani ya miguu yako.
Safari yako haikuwa rahisi mpaka sasa kwa kupewa majukumu kuibeba nyumba yako ya Ufaransa katika mgongo wako. Utabaki ndani yetu katika kipindi hiki. Natamani kulia kuona miguu yako sehemu ulipoiweka katika klabu yako ya West ham huku sura yangu ikibaki ndani yangu kumwona Theo Walcott akiwa ndani ya Emirates.
Walio na macho ya ziada watakuwa wameona, hiki unachokitoa kwa ajili yetu. Wewe ni mshindi wa kweli hata harufu ya miguu yako inanipa imani dhidi yako.
Ludivine Payet huyu ndie mwanamama kipenzi cha payet huyu ndiye mrembo aliye karibu na mumewe. Tabasamu lake usiku ule katika pambano lao waliokuwa wanacheza dhidi ya Albania kwa mumewe kulionyesha furaha dhidi yao.
Payet unazidi kutupa unachotaka, unazidi kutupa tunachostahili pia. Mboni za macho yangu zinazidi kuona utimilifu wako ndani ya miguu yako.
Namba hazidanganyi man of the match katika gemu mbili za mwisho katika taifa lako inazidi kutufanya kuamini kile ulichonacho kwa taifa lako.
Wakati mwingine nawaza kwanini miguu yako imechelewa kuchanua haraka. Tulitamani kuona ubora wa miguu yako ikiwahi kuchanua kwa haraka angalau ukiwa na umri wa miaka 22-26.
Kwakua dunia ilichelewa kuwa katika usawa hata wewe umechelewa kutuletea bidhaa yako mapema katika mboni za macho yetu. Umri wako wa miaka 29 tutakuwa na muda mchache sana wa kuona ubora wako utakaofichwa na umri wako.
ASANTE DIMITRI PAYET, ACHA NIFUNGE UKURASA WAKO.
No comments:
Post a Comment