HATUA ya Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe (ACT- Wazalendo) kuanzisha mjadala wa bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha nje ya Bunge, imekosolewa ukitajwa kwamba hauna tija zaidi ya kuwavuruga wananchi.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa, waliohojiwa jana, walisema kitendo hicho ni mkakati usio na tija huku wengine wakisema ni maoni ya kujifurahisha.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema kitendo hicho cha Zitto ni ‘mkakati usio na tija’. Naibu Katibu wa Bunge, John Joel alisema ‘ni maoni ya kujifurahisha’ wakati Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba alisema atajitokeza hadharani baadaye kutoa maoni ya kuliunganisha Taifa.
Baada ya kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge hivi karibuni kutokana na kukiuka taratibu, Zitto amekuwa akitumia majukwaa kukosoa bajeti na Serikali ya Rais John Magufuli, hatua ambayo imeelezwa pia kuwa inashusha heshima ya Mbunge huyo.
Warioba kufunguka Warioba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, alipotakiwa kutoa maoni yake kwa hatua hiyo, alisema wakati utakapofika atajitokeza na kueleza namna wanasiasa wanavyotumia vibaya nafasi zao za kisiasa.
“Kwa sasa tumekaa kimya, lakini wakati utafika ambapo tutajitokeza na kutoa maoni yetu kwa maslahi mapana ya taifa pamoja na kwamba tunaona namna wanasiasa wanavyotumia vibaya nafasi zao za kisiasa na kuligawanya Taifa. Kazi yetu sisi ni kuliunganisha taifa kuwa moja,” alisema Jaji Warioba.
No comments:
Post a Comment