Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akipokea Hundi ya mfano ya shilingi milioni kumi kutoka kwa mkurugenzi wa mawasiliano wa kampuni UR Group, Salim Omar, zilizotolewa na kampuni yake k ajili ya ujenzi wa Madawati kwa Shule za Msingi.
Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii.
SERIKALI imewataka wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini, kutumia fursa ya elimu bure kwa kujifunza kwa bidii ili taifa lijalo liweze kuwa wataalam wa kutosha kutokana na mazingira bora ya kusomea yamewekwa.
Hayo ameyasema leo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul alipokuwa akipokea mfano wa hundi ya sh. milioni 10 kutoka katika Kampuni ya Urban and Rural Engineering Services Limited (UR GROUP) kwaajili ya kuwezesha mpango elimu bure katika upande wa madwati.
Makonda amesema kuwa wanafunzi wasitumie fursa hiyo kama njia ya kubweteka bali waitumie kama mlango wa kutokea kwa kuja kuwa viongozi bora kutokana na mazingira waliosoma.
Amewataka wanafunzi hao kujifunza kwa bidii ili kujenga taifa la kesho lenye wasomi wengi ambao watakuwa viongozi kijamii na kitaifa.
Makonda aliipongeza kampuni ya UR Group kwa msaada walioutoa na kwamba umeongeza tija kwenye utoaji wa wa elimu bora nchini kwa kuunga jitihada za Rais Dk.John Pombe Magufuli.
“ katika msaada huu naamini i kutoa ni moyo wala sio utajiri na kila mwanafunzi anatakiwa kutambua kuwa tunapata misaada kutoka kwa watu kama nyie ili kuwafanikisha wao kusoma katika mazingira bora ya kusomea’’amesema Makonda.
Amesema bado mkoa una uhitaji wa madawati mengi kwaajili ya wanafunzi hasa kwa shule za msingi ambapo ndipo msaada umekuwa ukielekezwa zaidi maana ndio msingi wa elimu.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo,Ezekiel Sizya alisema kwakuona umuhimu wa shughuli zinazofanywa na serikali, wamesukumwa kuiunga mkono hasa katika suala zima la kuhakikisha wanafunzi wanasoma bure katika mazingira mazuri yakiwemo ya kukalia dawati wawapo darasani.
Sizya amesema huo sio mwisho kwao wa kuiunga serikali mkono bali wataendelea kujitoa kwa kile wanachokipata ili kuhakikisha kuwa nchi inafikia kiwango kizuri kiuchumi na kielimu.
“Tulichotoa kwaajili ya watoto wetu sio kikubwa lakini tunaamini tutakuwa tumewasaidia wanafunzi zaidi ya mia moja kutokaa chini badala yake watakalia madawati wawapo darasani,watanzania wenzangu wenye mapenzi mema kuendelea kujitoa kwaajili ya nchi yetu hasa suala zima la elimu ili kujenga taifa la wasomi,”amesema.
No comments:
Post a Comment