Timu mbili zenye nguvu katika kundi D, Croatia na Uhispania zinakutana leo katika mchezo wa kuhitimisha hatua ya makundi utakaochezwa majira ya saa 4 usiku kunako dimba la Nouveau Stade de Bordeaux uliopo manispaa ya Bordeaux.
Huu ni mchezo ambao unahusisha mataifa mawili yenye wachezaji wanaocheza vilabu vikubwa duniani. Ni mechi ambayo inatarajiwa kuwa na mvuto na msisimko wa hali ya juu ambapo inahisiwa kuna nafasi nyingi sana za magoli zitatengenezwa.
Ivan Ratikic na Luca Modric kwa upande wa Croatia ni wachezaji wenye kumulikwa sana huku Uhispania ikiwategemea nyota wake kama Andres Iniesta, Alvaro Moratta, Koke na wengineo.
Katika mchezo wao uliopita uliochezwa Ijumaa, Croatia walijikuta wakivutwa shati na Czech Republic kufuatia kulazimishwa sare ya 2-2, mchezo uliofanyika katika dimba la Stade Geoffroy-Guichard huko Saint-Étienne na kunyimwa nafasi ya kujihakikishia kufuzu moja kwa moja hatua ya 16 bora. Magoli ya nyota wa Inter Milan Ivan Perisic na Ivan Rakitic yalijikuta yalikosa umuhimu baada ya Milan Skoda na Tomas Necid kuisawazishia Czech katika muda wa majeruhi.
Croatia watakuwa kwenye hatihati ya kutofuzu kwenda raundi ya 16 endapo watapoteza mchezo huu dhidi ya Uhispania halafu Czech akashinda mchezo wake dhidi ya Uturuki.
Kwa upande wao, Uhispania ndio vinara wa kundi hilo wakiwa na pointi sita baada ya kushinda mechi zake zote mbili. Ushindi wa mchezo wao dhidi ya Uturuki ndio uliwapa tiketi ya kufuzu moja kwa hatua ya 16 bora.
Kocha wa Croatia Ante Čačić anaweza kupata pigo kwa kumkosa nyota wake Luka Modric ambaye aliumia katika mchezo dhidi ya Czech Republic.
Vile vile beki wake kati Vedran Corluka kuna wasiwasi wa kutocheza kufuatia kupata majeraha ya kichwa pia katika mchezo dhidi ya Czech.
Uhispania kwa upande wako wako sawa isipokuwa kocha wa timu hiyo Vicente del Bosque anaweza kufanya ‘rotatation’ ya kikosi chake kutokana na kujihakikishia kucheza hatua ya mtoano.
Sergio Ramos ana kadi ya njano hivyo anaweza kupumzishwa ili kuepuka kupata kadi nyingine itakayomnyima fursa ya kucheza mchezo muhimu katika 16 bora.
Rekodi ya michezo waliyokutana.
- Croatia wameshinda mchezo mmoja kati ya mitano waliyocheza na Uhispania (sare moja, wamefungwa mara tatu).
- Mchezo wao walioshinda, magoli yao yalifungwa na Roberto Prosinecki na Davor Suker mwaka 1994 jijini Valencia, ukiwa ni mchezo wao kwanza kushinda ugenini tangu kupata uhuru.
- Mchezo wao wa mwisho wa kimashindano kukutana ilikuwa ni wakati wa hatua ya makundi michuno ya Euro mwaka 2012. Goli la Jesus Navas katika dakika ya 88 lilitosha kuwaangamiza Croatia katika mchezo huo ambao walihitaji ushindi ili kufuzu.
Croatia
- Croatia wameshindwa kufunga mara moja tu katika michezo yao 11 kwenye michuano ya Ulaya. Mara ya mwisho kushindwa kufungwa ilikuwa mwaka 2012 walipofungwa na Uhispania.
- Croatia wamepiga jumla ya mashuti 20 katika michezo yao yote miwili ya mwanza, mengi zaidi ya wapinzani wao.
- Croatia wameshinda mchezo mmoja tu katika mashindano mbalimbali ambapo Luka Modric hakucheza tangu alipoanza kucheza kwa mara ya kwanza mwaka 2006. Ilikuwa ni dhidi ya Poland katika michuano ya Euro mwaka 2008. Alikuwa amepumzishwa katika mchezo huo kutokana na timu yake kuwa tayari imefuzu.
- Ivan Perisic amehusika katika magoli mawili kwenye michezo mitani iliyopita (goli moja, assist moja)
- Nahodha Darijo Srna anatarajia kucheza mchezo wake wa 17 katika michuano mbalimbali, anaweka rekodi mpya kwa taifa hilo.
Uhispania
- Uhispania hawajafungwa kwenye michezo 14 katika michuano ya Ulaya (wameshinda mara 11, sare mara 3).
- Hawajaruhusu goli lolote kwa takriban dakika 690 katika michuano mbalimbali.
- Uhispania wameruhusu goli moja tu katika michezo yao 11 ya mwisho ya michuano ya Ulaya. Goli hilo lilifungwa na Antonio Di Natale June 10 mwaka 2012 wakati walipotoka sare ya bao 1-1 na Italy.
- Andres Iniesta amepiga pasi zilizofanikiwa 177 katika michuano ya Euro mwaka huu, zaidi ya mchezaji yeyote wa Uhispania.
No comments:
Post a Comment