John Magufuli, Rais wa Tanzania
RAIS John Magufuli leo akiwa Ikulu, jijini Dar es Salaam ameonesha kukerwa na mihadhara ya kisiasa nchini na kuhoji, “watu watakula wapi?” anaandika Hamisi Mguta.
Kumekuwepo na mvutano kati ya Jeshi la Polisi na vyama vya siasa hususan vya upinzani baada ya kutolewa tangazo la kuzuiwa mikutano na maandamano ya kisiasa nchini.
Hatua hiyo imesababisha kuibuka kwa mgogoro huku Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema pia mwenyekiti mwenza wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akifungua kesi mahakamani kuwashitaki baadhi ya viongozi akiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali .
Wakati akipokea taarifa ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Rais Magufuli amesema, baada ya kufanyika uchaguzi kinachofuata ni maendeleo.
Ameeleza kuwa, kila nchi baada ya uchaguzi kuisha kinachofuata ni kutekeleza ahadi na kwamba, haiwezekani muda wote iwe ni kufanya siasa.
Amehoji, kama siasa ikifanyika kila siku watu watakula wapi? “Haiwezekani kila siku ni siasa, watu watakula wapi?”
Hata hivyo amesema, hayuko tayari kuona mtu yoyote katika utawala wake akichelewesha safari yake ya mafanikio katika miaka yake mitano ya utawala.
Amesema, serikali inayoongoza nchi sasa ni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na yapo waliyoahidi katika kipindi cha miaka mitano ambayo anapaswa kuyatekeleza.
“Wanasiasa wafanye sasa kwa ushindani wote, iwe madiwani wapeleke hoja ngumu kwa wananchi au wawakikishi wa wananchi ili baada ya miaka mitano wananchi wahoji tuliyoyatekeleza na kushindwa kuyatekeleza,” amesema.
Aidha, amesema NEC imefanya kazi nzuri kusimamia uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana na kwamba, taasisi hiyo imerahisishia kuendelea na majukumu yake vizuri.
Hata hivyo ameieleza NEC kuwa, suala la ujenzi wa ofisi maalum ya tume lipo pale pale kwa mapendekezo ya kwamba, ofisi hiyo ijengwe Dodoma ili kutimiza lengo la Mwalimu Julius Nyerere la serikali kutoka kuhamia huko.
“Kama mapendekezo yangu yatakubaliwa basi tutaweza hata kupunguza msongamano wa foleni Dar es Salaam,” amesema.
Ujenzi huo wa ofisi za NEC ni ule ulioelezwa kutekelezwa kupitia Sh. 12 bilioni ambazo ilirudishwa na Damian Lubuva, Mwenyekiti wa NEC wiki chache zilizopita baada ya fedha hizo kutotumika Uchaguzi Mkuu.
Amesema, cheo cha rais ni msalaba aliotwikwa na wananchi lakini bado ushirikiano na wanasiasa wenzake upo palepale.
“Ili nchi isonge mbele, lazima kuiweka nchi na maendeleo ya watu kwanza kisha vyama baadaye. Uongozi ni msalaba hivyo unahiyaji msaada wa Mungu,” amesema.
No comments:
Post a Comment