LONDON, UINGEREZA – Katika hali inayoonesha kumomonyoka kwa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya wananchi wa Uingereza jana Alhamisi wamepiga kura ya maoni kutaka taifa lao lijitoe kwenye Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) ikiwa ni pigo kubwa kwa Waziri Mkuu David Cameron, wafanyabiashara na wasomi wengi wa taifa hilo. Wapiga kura wengi zaidi walijitokeza kupiga kura ya maoni kuliko ilivyokuwa kwenye uchaguzi mkuu uliopita. Inakadiriwa zaidi ya asilimia 70 ya wapiga kura wamejitokeza kupiga kura. Kura ya kubakia ilitarajiwa kupigwa na maeneo ya miji mikubwa hata hivyo, inaonekana kwenye baadhi ya miji hiyo kura ya kujitoa imeshinda kinyume cha matarajio ya wengi.
Uamuzi wa kuitisha kura ya maoni ulichukuliwa baada ya mijadala mikali ya wanasiasa na wananchi ambao waliona kuwa Umoja wa Ulaya umekuwa ni tishio la utambulisho, historia, na maslahi ya Waingereza kwa muda mrefu na kuendelea kufungwa na mikataba mbalimbali ya umoja huo hakukuwa na manufaa makubwa kwa Waingereza kuliko kuwa nje ya Umoja huo.
Waziri Mkuu Cameron alitangaza mwezi Februari kuwa Juni 23 itakuwa ni siku ya kupiga kura ya maoni ili wananchi wa Uingereza wapate nafasi ya kutoa kauli yao juu ya kuendelea au kutoendelea kuwemo ndani ya Umoja wa Ulaya.
Matokeo ya kura hiyo ya maoni kwa yanaonesha kuwa asilimia 52 ya wapiga kura wa Uingereza wameamua nchi yao ijitoe wakati asilimia 48 walikuwa wanataka ibakie. Taratibu za kuelekea kujitoa kwenye jumuiya hiyo zitaanza mapema iwezekananavyo na wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanaamini ndani ya miaka miwili ijayo Uingereza itakuwa nje ya Jumuiya hiyo. Matokeo kamili yatajulikana baadaye leo hii.
Hata hivyo, matokeo ya kura hii yanahofia kuwapa nguvu na mori wananchi wan chi nyingine wanachama ambao nao wanaweza kuanza kutaka wapige kura ya maoni na hivyo ukawa mwanzo wa jumuiya hiyo kuvunjika. Hisia za watu kutokufurahia maamuzi ya Jumuiya hiyo kutoka kwenye makao yake makuu huko Brussels, Ubelgiji ni pamoja na masuala ya uhamiaji ambapo wananchi wengi wa Ulaya wanaona sera za kuruhusu wahamiaji zinatishia maisha ya baadaye ya nchi wanachama hasa ujio wa wahamiaji kutoka nchi zenye migogoro za Mashariki ya Kati.
Pamoja na masuala ya uhamiaji masuala mengine ambayo yanaonekana kuwakwaza Waingereza wengi ni masuala ya kiuchumi ambayo yanaonekana kubebesha mzigo mkubwa kwa nchi kama Uingereza na Ujerumani kutumia uwezo wake kusaidia nchi zenye matatizo ya kiuchumi. Hata hivyo, wafanyabiashara na makampuni mengi makubwa ya Uingereza yalikuwa yanaunga mkono kampeni ya kubakia ndani ya Jumuiya hiyo. Mapema asubuhi hii matokeo ya kura hii yalivyozidi kuonesha kuwa waliotaka kujitoa wanaelekea kushindi masoko mbalimbali ya hisa duniani yameitia kwa kusababisha thamani ya paundi ya Kiingereza kushuka kwa mteremko mkubwa ambao haujawahi kutokea katika miaka zaidi ya thelathini.
Waziri Mkuu Cameron mwenyewe alijikuta ameshindwa kushawishi chama chake mwenyewe kuongoza kampeni ya kubakia na zaidi ya nusu ya wabunge wake walikuwa wanaunga mkono kampeni ya kutoka EU. Kuna uwezekano mkubwa kuwa Waziri Mkuu Cameron akaamua kujiuzulu nafasi yake kufuatia kipigo hicho kutoka kwa wapiga kura. Utaratibu wa kiongozi wa chama kuachia ngazi anaposhindwa uchaguzi (uwe uchaguzi mkuu wa kura ya maoni) ni wa kawaida katika nchi za kidemokrasia kwani mapendekezo yake ya kisiasa yanakuwa yamekataliwa na hivyo anatoa nafasi kwa kiongozi mwingine kushika hatamu ya uongozi.
Kiongozi wa kampeni ya kujitoa Bw. Nigel Farage ni kutoka chama cha Independent ambacho ni miongoni mwa vyama vidogo vya Uingereza lakini ambaye amekuwa na ushawishi mkubwa katika kampeni hii.
Mojawapo ya sauti ambazo zinasubiriwa kusikiwa ni jinsi gani Serikali ya Marekani itaupokea uamuzi wa kura hii ya maoni kwani kwa muda mrefu Marekani imekuwa ikiamini Uingereza ina nafasi nzuri zaidi ndani ya jumuiya hiyo ya Ulaya kuliko nje yake. Rais Obama mwenyewe miezi miwili iliyopita alifunga safari kwenda Uingereza ambapo alitumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi wa Uingereza kupiga kura ya kubakia ndani ya jumuiya hiyo.
Mwitikio mwingine ambao unasubiriwa kusikilizwa ni kutoka Scotland, sehemu ya Ufalme wa Uingereza ambayo miaka michache nyuma ilipiga kura ya kuamua kubakia ndani ya Muungano wa Uingereza na katika kura hii kwa kiasi kikubwa walitaka Uingereza ibakie ndani ya EU. Tayari baadhi ya watu mashuhudi wameanza kutaka Scotland irudi tena kwenye kura ya maoni na wanaweza kutaka wajitoe ili wao waendelee kuwa sehemu ya EU.
No comments:
Post a Comment