Diwani wa kata ya Miono ,wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani ,Juma Mpwimbwi ,akizungumzia juu ya tatizo la njaa katika baadhi ya maeneo ya kata hiyo kwa mbunge wa jimbo la chalinze Ridhiwani Kikwete ,aliye kushoto kwa diwani huyo.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
NA Mwamvua Mwinyi DIWANI wa kata ya Mioni ,jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ,Juma Mpwimbwi amemuomba mbunge wa jimbo hilo Ridhiwani Kikwete ,kuvalia njuga tatizo la njaa ambalo limewakumba baadhi ya wananchi katika kata hiyo.
Amesema kwasasa hali ni ngumu hususan katika vijiji vya Masimbani na Kwaikonje ambapo ni miaka mitatu mfululizo sasa hawana chakula huku misimu ya kilimo ikiwa imebadilika hivyo hawana hata vibarua vya kulima .
Mpwimbwi amemuomba mbunge huyo kusimamia suala hilo ili kunusuru familia ambazo zinaishi kwa shida bila chakula.
Akizungumza juzi,mbele ya mbunge wa jimbo hilo,pamoja na baadhi ya wananchi katika kata hiyo, Mpwimbwi alisema uhaba wa chakula upo zaidi maeneo ya pembezoni mwa kata .
“Ni afadhali ya sisi tunaoishi hapa mjini mjini maana mtu anaweza akamwomba mwenzie hata sembe ama kuuza mkaa wake kwa sh.1,500 kwa kiroba cha kilo 25 licha ya kuzoeleka kuuza mkaa huo kwa sh.5,000”
"Imefikia hatua nawakimbia watu,mtu akija kuniulizia nyumbani kwangu inabidi waambiwe sipo,kwakuwa mimi mwenye hela ya kusaidia watu wote sina na najisikia vibaya kuona mtu ananifuata halafu nimwambia hela ama chakula cha kumpa sina"alisema Mpwimbwi.
Nae Ridhiwani alisema anatambua tatizo hilo linalowakabili wakazi hao na kusema taarifa tayari ipo kwa waziri mkuu Kassim Majaliwa na wakati wowote kuanzia sasa chakula cha msaaada kitapelekwa kwa walengwa.
Alieleza kuwa mwishoni mwa wiki iliyopita aliongea na waziri mkuu ambapo alimwambia kuwa katibu tawala mkoa(RAS)ameshapeleka taarifa yake ya uhakiki ambapo kwa wilaya ya Bagamoyo mahitaji ya chakula yanayotakiwa ni tani 4,369.
Hata hivyo Ridhiwani alisema hivi karibuni viongozi na watendaji wa vijiji wote walipewa agizo la kuhakikisha wanaandika mahitaji ya chakula na kisha kuipeleka ngazi ya wilaya ,mkoa na kwa waziri mkuu.
“Kila zama na kitabu chake ,inabidi tukubaliane na hili kwani ilitakiwa kujiridhisha na taarifa zilizotolewa kabla ya kufanya maamuzi ili kuepukana na tatizo lililokuwepo zamani la baadhi ya watendaji kuzidisha tani 5 kumbe ni tani mbili za chakula “
“Lakini hatua zinachukuliwa kwani taarifa zilishakwenda kwa waziri mkuu akaagiza kufanyika uhakiki kwanza kwa wilaya kujiridhisha na taarifa huku uhakiki ukionyesha kuwa ni tani 4,369 zinazohitajika kiwilaya”alisema Ridhiwani.
No comments:
Post a Comment