RC SINGIDA AWABANA VIONGOZI WA WILAYA YA SINGIDA. - PATRICIA-TV.com

Breaking

Share daily activities and have all funs here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Thursday, June 23, 2016

RC SINGIDA AWABANA VIONGOZI WA WILAYA YA SINGIDA.

IMG_4286
Mkuu wa Mkoa wa Singida

Serikali ya mkoa wa Singida, imeiagiza halmashauri ya wilaya ya Singida kulipa michango ya hifadhi ya jamii iliyokatwa kutoka kwenye mishahara ya watumishi, ndani ya wiki moja kuanzia Juni, 23 mwaka huu.

Agizo hilo limetolewa na mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe,wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao maalum cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo. Kikao hicho kiliitishwa kwa ajili ya kujadili taarifa ya matokeo ya ukaguzi na majibu ya hoja za mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali kwa kipindi cha kuishia Juni, 30 mwaka jana.

Alisema kushindwa kuwasilisha michango ya watumishi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wakati ni kinyume na sheria za nchi zinazotaka michang hiyo kuwasilishwa kwa muda sahihi.

“Athari ya kutokuwasilisha michango ya watumishi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wakati, halmashauri hii inaweza ikatozwa tozo za riba bila sababu za msingi,” alisema mkuu huyo wa mkoa.

Kutokana na hali hiyo, Mhandisi Mtigumwe alimwagiza mkuu wa wilaya ya Singida kusimamia kwa karibu zoezi la kuwasilisha michango ya watumishi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ndani ya siku 14 na si vingenevyo.

Aidha, ameiagiza halmashauri hiyo iangalie uwezekano wa kutenga bajeti ya kuajiri madereva ambao kwa sasa wanafanya kazi hiyo, kwa masharti ya muda wanaodai mishahara ya zaidi ya shilingi 11.6 milioni.

“Kuchelewa kuwalipa watumishi haki zao kunaweza kuzorotesha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuteteresha ustawi wa jamii na ya watumishi pia. Zingatieni kutoa haki za watumishi hasa mishahara kwa wakati,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa mkoa, alisema ingawa halmashauri hiyo ilikuwa nyuma katika zoezi la madawati, lakini kwa sasa inakwenda vizuri, na kuna kila dalili kwamba itamaliza tatizo la upungufu wa madawati kabla ya muda uliopangwa.

“Kwa hili nawapongeza sana, lakini niwaombe waheshimiwa madiwani, mkurugenzi mtendaji na watendaji wote kwa ujumla, mjipange vizuri zaidi kuhakikisha mnaondoa mapungufu yaliopo kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo ukusanyaji duni wa mapato ya ndani,” alisema na kuongeza kwa kusema.

“Nina wasi wasi sana na watendaji wa halmashauri hii, nawasihi mbadilike haraka na mhakikishe kila mmoja anakwenda sambamba na kasi ya utendaji ya serikali ya awamu ya tano, tofauti na hivyo, itakula kwako”.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Elia Digha, amewataka watendaji wahakikishe wanajipanga vema, ili kuondokana na hoja zinazoisababishia halmashauri kupata hati yenye shaka.

“Kwa kipindi cha miaka minne (kuanzia mwaka wa fedha wa 2010/2011 hadi 2013/2014), halmashauri yetu imekuwa ikipata hati safi. Vipi tena mwaka wa fedha wa 2014/2015 tumeweza kurudi nyuma na kupata hati yenye shaka … kumekuwa na hoja 107, hii haikubaliki kabisa. Lazima tujipange na kurekebesha upungufu huu,” alisema Digha ambaye ni diwani (CCM) wa kata ya Msange.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here