Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI imetiliana saini kuzinunua rasmi hisa asilimia 35 za Kampuni ya Bharti Airtel Afrika ndani ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ikiwa ni hitimisho la kuimiliki TTCL kwa asilimia 100 hivi sasa.
Tukio hilo lilifanyika Dar es Salaam jana ambako Serikali iliwakilishwa na Msajili wa Hazina, Laurence Mafuru huku kampuni ya Bharti Airtel Afrika ikiwakilishwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Christian de Faria.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kutiliana saini, Mafuru, aliishukuru Kampuni ya Bharti Airtel kwa kukubali kuuza hisa zake na kuirejeshea Serikali umiliki wa asilimia 100 ndani ya TTCL.
“Zipo sababu za biashara na maslahi mapana ya nchi ambayo yametuongoza kufikia hatua hii muhimu. Ni imani ya Serikali kuwa, baada ya kusaini nyaraka hizi zinazohitimisha ubia wa kampuni hizi, tutaiona TTCL mpya iliyo na kasi na viwango vya hali ya juu vya huduma kwa wananchi sambamba na kujiendesha kwa biashara na kutoa gawio kwa Serikali yenye malengo na matarajio makubwa sana kwa kampuni hii,” alisema Mafuru.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa a Bharti Airtel Afrika, De Faria alisema kampuni yao inayo furaha kubwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuinua mchango wa sekta ya mawasiliano katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi wake.
“Tumeshirikiana kwa muda mrefu na tunaamini tutaendelea kuwa pamoja katika kuikuza sekta ya mawasiliano nchini Tanzania. Tunaishukuru Serikali na TTCL kwa kutekeleza makubaliano yetu na kuhitimisha ubia huu,” alisema kiongozi huyo wa Bharti Airtel.
Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Profesa Tolly Mbwete, alisema kuhitimishwa kwa ubia huo wa biashara kati ya TTCL na Bharti Artel kunaleta faraja kubwa kwa uongozi wa TTCL.
“Tumesubiri kwa muda mrefu taratibu za mchakato huu zikamilike, hatimaye siku imewadia. Pamoja na shukrani za dhati kwa Serikali na wenzetu wa Bharti Airtel kwa kufanikisha mchakato huu.
“… nirudie wito wangu kwa menejimenti na wafanyakazi wa TTCl, sasa kumekucha. Ni wakati wa kuonyesha kwa vitendo uwezo na uzalendo wetu katika kutekeleza mipango yetu ya biashara na ndoto yetu kuwa mhimili na kinara wa sekta ya mawasiliano nchini,” alisema Profesa Mbwete.
No comments:
Post a Comment