HUKUMU ya kesi ya ubunge katika Jimbo la Longido mkoani hapa itarajiwa kutolewa Juni 29, mwaka huu na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba anayesikiliza kesi hiyo, Sivangilwa Mwangesi alisema hayo juzi mara baada ya msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo hilo, Felix Kimario kumaliza kutoa ushahidi wake na upande wa mwendesha mashitaka wa serikali kusema wamefunga ushahidi.
Aliwaagiza Mwanasheria wa Serikali, David Akway na Neema Mwanga na mawakili wa mlalamikaji mgombea wa CCM, Dk Stephen Kiruswa, Masumbuko Lamwai, Edmund Ngemela na Daudi Haraka kuwasilisha utetezi wao Juni 23 mwaka huu bila ya kukosa.
Alisema utetezi wa pande zote unapaswa kuwa wa maandishi ili ndani ya siku tano awe ameusoma na hatimaye kutoa hukumu Juni 29 mwaka huu .
“Fanyeni kila mnaloweza ili utetezi wenu unifikie kabla ya Juni 23, mwaka huu maana kesi nataka kumaliza kabla ya Juni 29 mwaka huu siku hiyo nitatoa hukumu ya kesi hii kwani nimekaa sana Arusha,” alisema.
Awali kabla ya kuahirisha kesi hiyo msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Longido, Kimario (58) ambaye alikuwa shahidi wa 13 katika kesi hiyo aliieleza Mahakama kuwa katika chumba cha majumuisho kulikuwa na vurugu, lakini hazikumzuia yeye kuacha kuendelea na shughuli za majumuisho ya kura za vituo 175 vya jimbo hilo.
Kimario ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Longido alisema hayo wakati akihojiwa na Wakili John Materu anayemtetea mjibu maombi namba moja wa kesi hiyo, Mbunge wa Chadema, Onesmo ole Nangole mbele ya Jaji Mfawidhi Mwangesi.
Alisema katika chumba cha majumuisho kilichoko katika majengo ya Halmashauri ya Longido kulikuwa na vurugu za kurushiana maneno ya pande mbili za wafuasi wa Chadema na wafuasi wa CCM.
Alisema vurugu ambazo hazikuathiri shughuli za kuhesabu kura za vituo vyote 175 vya jimbo hilo hakuna mtu aliyeamuru atolewe nje ya ukumbi.
Shahidi huyo alikiri pia kuwepo kwa kasoro katika mahesabu ya majumuisho na hiyo ilitokana na wahusika katika idara ya mfumo wa kompyuta wa tume kuchoka na kuwa na usingizi, kwani walifanya kazi hadi alfajiri .
Wakili Materu alimuuliza shahidi kama kulikuwa na malalamiko yoyote katika kipindi cha kampeni na kipindi cha uandikishaji kura, shahidi Kimario alisema yeye kama msimamizi mkuu hakuwahi kupata malalamiko yoyote kwa wagombea wowote wa siasa wa jimbo hilo.
Mkurugenzi huyo alisema pia kuwa katika chumba hicho hakuwahi kumtoa mtu yoyote nje ya ukumbi kutokana na vurugu wala kosa lolote ila alikiri kuhojiwa polisi juu vurugu katika chumba cha majumuisho.
Alisema mbali na yeye hata Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Longido (OCD) hakumtoa mtu katika ukumbi huo kwa kosa la vurugu.
Wakili Materu alimuuliza shahidi kuwa yeye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hivyo anaitaka Mahakama hiyo iamue nini kutokana na ushahidi wako ambapo aliiomba kesi hiyo itupiliwe mbali na mshindi abaki yule yule aliyemtangaza, yaani Nangole.
Shahidi huyo alisema kuwa mgombea wa CCM, Dk Kiruswa na wenzake walitoka nje ya ukumbi wa majumuisho muda mfupi kabla ya kumaliza shughuli za kuhesabu kura za vituo vyote.
No comments:
Post a Comment