Na Zainab Nyamka,Globu ya Jamii.
KUTOKANA na mkanganyiko wa uendeshaji wa mchakato wa uchaguzi katika Klabu ya Stand United ya Shinyanga, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF), limeagiza michakato yote miwili inayoendeshwa sambamba ndani ya klabu ya Stand United, isimamishwe mara moja kisha kusubiri maelekezo mengine.
Hilo limekuja baada ya kuwa na sintofahamu kwa pande mbili tofauti kufanya uchaguzi kwa nyakati tofauti moja ikiwa Kampuni na wengine wakijiita wanachama wa Stand United.
Akizungumza na Globu hii, Mkurugenzi wa Ufundi Muhibu Kanu kwa niaba ya Stand United Kampuni amesema kuwa wamesitisha uchaguzi huo mpaka pale watakapopewa angalizo na TFF kwani wao wanafahamu mchakato mzima jinsi ulivyo ndani ya klabu hiyo pamoja na hao wanaojiita wanachama. "Tumepokea barua kutoka TFF ikituambia kuwa tuache mchakato wa uchaguzi na sisi tumetii kwani tunachofahamu sisi ndiyo wenye haki na mamlaka zaidi tunachosubiri ni maamuzi yao".
Kanu amesema, baadhi ya watu hawaitakii mema klabu hiyo zaidi wanachotaka ni kuona ni kila siku kuwa katika migogoro itakayokuwa haina manufaa na kudhoofisha maendeleo, kitu ambacho si kizuri na wanachotakiwa ni kuacha uongozi unaotambulika kufanya kazi yake kwa ufasaha na kuitoa timu mahala ilipo na kuipeleka juu Zaidi.
"Wanachoona ni kuwa timu imepata mdhamini na ametaka kuleta maendeleo kwenye klabu yetu wanaanza kujitokeza kwa kuanzisha mchakato wa uchaguzi na wakijiita wanachama wa Stand ilihali kuwa wanafahamu kuwa kwa sasa tumesajili kama kampuni na wale wanachama wote wa halali tulioanza na timu tulikaa chini kwenye mkutano mkuu na kukubaliana kwa pamoja,"amesema Kanu.
No comments:
Post a Comment