Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) limesema litaingilia kati suala la mchezaji Ramadhan Kessy aliyesajiliwa na Yanga huku Simba wakikataa kuiandikia barua Yanga kumruhusu mchezaji huyo kuanza kuitumikia klabu hiyo.
Alfred Lucas
CAF iliizuia Yanga kumtumia Kessy katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi kombe la shirikisho barani Afrika CAF CC mpaka pale Simba itakapoandika barua ya kuiruhusu Yanga kumtumia mchezaji huyo.
Tayari Yanga imeiandikia barua klabu ya Simba juzi na nakala kuiwasilisha TFF wakihoji kama kuna pingamizi lolote juu ya mchezaji huyo ambaye mkataba wake na klabu ya Simba unafikia kikomo Juni 30.
Ofisa habari wa TFF, Alfred Lucas amethibitisha kupokea nakala ya barua hiyo kutoka kwa Yanga kwenda kwa Simba huku akisema kuwa wanalifuatilia suala hilo.
"Tusingeweza kuingilia kati suala hili mpaka Yanga wenyewe waiandikie Simba kuomba ruhusa yao na kama Simba watachelewa kuwajibu Yanga, sisi tutaingilia kati kwa kuwapa taarifa CAF kuwa Kessy hana mkataba na Simba na aruhusiwe kuichezea Yanga" alisema Lucas
Aidha msemaji huyo aliongeza kuwa mchezaji akibakiza muda fulani wa mkataba wake anaruhusiwa kujiunga na klabu yoyote na ndivyo ilivyo kwa Kessy.
Hata hivyo Lucas aliishutumu klabu ya Yanga kwa kushindwa kutuma mtu kuhudhuria semina maalumu iliyoandaliwa na CAF kwa ajili ya mashindano hayo ambayo kwenye simina hiyo wangepata elimu juu ya mambo mbalimbali.
"Inashangaza sana CAF waliwatumia Yanga baura ya mwaliko mapema sana na mwenyekiti wao Yusuph Manji alithibitisha kupokea barua hiyo lakini wakaipuuzia. Wangetuma mtu kwenye semina ile ambayo CAF walikuwa wanagharamia kila kitu wangepata elimu kubwa ya ushiriki wao kwenye mashindano yao." alisema Lucas
No comments:
Post a Comment