VARGAS MILELE CHINI YA KIVULI CHA SANCHEZ CHILE - PATRICIA-TV.com

Breaking

Share daily activities and have all funs here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Sunday, June 19, 2016

VARGAS MILELE CHINI YA KIVULI CHA SANCHEZ CHILE

Vargas and Sanchez
Hakika hivi sasa Eduado Vargas anabidi awe ameshazoea kuishi nyuma ya kivuli cha Alexis Sanchez. Wote wawili hawa waliweza kujipatia magoli mawili kwenye ushindi wa Chile wa 4-2 dhidi ya Panama na kumaliza ukame wa magoli wa miezi nane ambao ulikuwa unawaandama wote wawili wakichezea timu yao ya Taifa. Lakini Sanchez ndiye aliyepata sifa zote kutokana na magoli yake mazuri aliyofunga kwenye mechi hiyo na kuhakisha kwamba anazidi kuinyemelea rekodi ya mfungaji bora kwenye historia ya nchi yake kwa kufanya  hivyo.
Vargas na Sanchez wote walianza kucheza mpira katika klabu ya Cobreloa ambayo ni klabu ndogo kwenye mji wa uchimbaji madini Calama ambayo ina tatizo kubwa la ukosefu wa pesa. Lakini njia zao hawa ni tofauti sana.
Sanchez hata alipokuwa mdogo alikuwa anasakwa sana na klabu kubwa mbalimbali nchini Chile na alichezea kwenye klabu za vijana za Universidad de Chile na Deportes Antofagasta kabla ya kujiunga na Cobreloa wakati Vargas alihangaika hapa na pale akicheza kwenye mashindano madogo ya Vijana na hata alishiriki kwenye kipindi cha Luninga kabla ya kusajiliwa na Cobreloa akiwa na miaka 16.
Akiwa na umri huohuo lakini mwaka kabla, Sanchez alikuwa tayari kati ya wachezaji wadogo zaidi kushiriki kombe la Copa Libertadores ambalo ni kombe kubwa sana Amerika ya Kusini. Wakati Vargas anapata nafasi ya kucheza timu ya kwanza kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 18, Sanchez yeye alishaanza safari yake ambayo hatimaye iliweza kumfikisha katika klabu kubwa za Barcelona 2011 na Arsenal 2014 tena akinunuliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha.
Vargas nae alinga’aa kwenye timu ya Cobreloa vile vile ila alichukua muda mrefu sana kuzoea mazingiria alipofika Universidad de chile. Hadi  leo hii ameshindwa kujitengenezea nyumbani barani Ulaya tangu ahamie klabu ya Napoli 2012.
Amechezea klabu mbalimbali kwa mkopo kama vile Gremio, Valencia na QPR. Alisajiliwa mwaka 2015 na klabu yake ya sasa Hoffenheim
Lakini kuna Idara moja ambayo wachezaji hawa huwa sawa….timu yao ya Taifa.
Sanchez yeye alifika hapa kwanza kwani aliitwa kwa mara ya kwanza kwenye timu ya taifa mwaka 2006 na akafanikiwa hata kucheza kombe la dunia mwaka 2010 chini ya Marcelo Bielsa.
Lakini Vargas nae alikuja kuwa mchezaji muhimu kama Sanchez kwenye timu ya Taifa baada ya kuajiriwa kocha wake wa Zamani katika klabu ya Universidad de Chile Jorge Sampaoli mwishoni wa mwaka 2012. Walipochezeshwa wote wawili kule mbele, uelewano wa Sanchez na Vargas ulikuwa msingi wa mafanikio ya timu ya Chile chini ya kocha wao Jorge Sampaoli.
“Wanacheza kama vile wanatoa kwenye kumbukumbu zao,” alisema Sampaoli mapema mwaka huu “yani ilichukua siku mbili tu kwa kila mmmojawao kuelewa harakati za mwenzake.”
Kilele cha mafanikio yao kilikuja kwenye Copa America ya mwaka jana pale Chile ilipoweza kutwaa taji lao la kwanza la kimataifa. Sanchez aliweza kupata heshima ya kupiga Penati ya mwisho iliowapa ushindi dhidi ya Argentina, lakini Vargas ndiye aliyetoa mchango mkubwa zaidi kwani ni yeye aliyefunga magoli mawili yaliyomtoa Peru kwenye nusu fainali ngumu.
Na kama unakumbuka vizuri katika kombe la Dunia la mwaka 2014 Vargas alikuwa mojawapo ya wachezaji bora katika michuano hiyo na alifunga goli la kwanza la Chile katika mechi yao dhidi ya Spain ambalo lilisaidia kumpeleka Chile kwenye hatua ya mtoano ya michuano hiyo huku Spain akirudi nyumbani.
Lakini ujio wa Juan Antonio Pizzi aliyechukua nafasi ya Sampaoli mapema mwaka huu uliweka uelewano wao katika hatihati. Vargas alikuwa amefungiwa kwenye mechi za kwanza za Pizzi kama kocha na aliporudi kwenye timu hiyo katika maandalizi ya Copa America Centenario alikutana na kocha ambaye hakuamini uwezo wa Vargas kucheza kama mashambuliaji. Vargas aliwekwa winga ya kulia katika kichapo cha 2-1 dhidi ya Jamaica mwezi uliopita  na aliwekwa hapohapo tena kwenye mechi ya ufunguzi dhidi ya Argentina. Katika mechi ya pili dhidi ya Bolivia, Vargas alijikuta akisugua benchi.
Lakini mihangaiko ya huyu kocha mpya katika safu yake ya ushambuliaji hatimaye ilimleta tena kwa Vargas na Sanchez katika ushindi dhidi ya Jamaica japo sasa hivi ni sehemu ya washambuliaji watatu na si wawili tena.
Magoli mawili ya Vargas katika hiyo mechi yalimfanya asogelee zaidi katika rekodi ya mfungaji bora wa Chile akiwa sasa katika nafasi ya tano na magoli 30, magoli 3 tu nyuma ya Alexis Sanchez aliyekuwa nafasi ya tatu.
Lakini daima Alexis Sanchez, Arturo Vidal na Gary Medel ndiyo wachezaji watakaopata sifa zote wakifuata kwenye nyayo za nyota wa zamani wa chile kama Ivan Zamorano na Salas. Wachezaji wote kwenye kikosi  cha 23 kilichotwaa Copa America mwaka jana wanastahili nafasi yao kwenye historia ya timu ya Chile ila Vargas anastahili zaidi.
Labda kinachomzuia ni ukosefu wake wa ile ‘amsha-amsha’ waliyokuwa nayo washambuliaji wengi waliozoleleka na kupendwa kwenye timu ya Chile kama wakina Zamorano na hata Sanchez kwa sasa hivi. Mpira wake yeye ni wa kimya zaidi, yeye hutegemea kujiweka katika sehemu nzuri uwanjani na kusubiri nafasi pale inampofikia.
Kitu kingine kinachomuangusha ni kushindwa kwake kufanya vizuri katika klabu zake mbalimbali alizochezea. Katika  misimu minne iliyopita katika klabu nne tofauti Vargas ameweza kufunga magoli 14 pekee katika mechi 80. Bila shaka kuchezeweshwa katika nafasi ya winga katika klabu hizi inachangia sana kwa hili.
Vargas ni mkimya sana na hajaonesha dalili yeyote kwamba anakereka na umaarufu wanaopata wachezaji wenzake ukilinganisha na  yeye. Baada ya matatizo aliyopata na kocha wake wa Sasa Pizzi mapema mwezi huu hakika  Vargas sasa atakuwa na furaha  hata kuchukua nafasi yake tu katika timu ambayo pia ina wakina Medel, Vidal na Sanchez. Vargas kama ilivyokuwa kawaida yake, anafanya mambo yake kimyakimya akitafuta nafasi na atapoipata bila shaka ataiweka golini na kuendelea kuisogeza Chile mbele kwenye michuano hii.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here