USHIRIKA wa Wachungaji wa Pentekoste Tanzania (PPFT), umeiomba serikali kumchukulia hatua za kisheria Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima (pichani) kwa lugha za uchochezi na uchonganishi, anazozitoa akiwa kanisani mwake.
Pia, walidai askofu Gwajima anataka kuhatarisha amani na utulivu uliopo nchini kutokana na kauli zake dhidi ya viongozi wa kitaifa, akiwamo Rais John Magufuli. Mwenyekiti wa PPFT, Askofu Pius Ikongo alisema hayo wakati akielezea msimamo wa ushirika huo, kutomuunga mkono Askofu Gwajima kulingana na kauli zake, akidai ni msimamo wa Wakristo nchini.
Askofu Ikongo alisema Askofu Gwajima amekuwa akitoa kauli za kuudhi dhidi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais mstaafu Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuwa wapo wanaCCM wanaozunguka nchini, kutaka asimkabidhi uenyekiti Rais Magufuli.
Pia alidai askofu huyo anatoa kauli za kumtaka Rais Magufuli, kumuondolea kinga ya kutoshtakiwa Kikwete ili afikishwe mahakamani kulingana na makosa mbalimbali wakati wa utawala wake.
Askofu Ikongo alisema kauli hizo Askofu Gwajima, amedai akizitoa kwa niaba ya Wakristo nchini licha ya kwamba matamko hayo, hayatambuliwi na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na maaskofu wa Makanisa ya Kipentekosti Tanzania (CPTC).
“Jumuiya ya Wachungaji inawaomba Watanzania kutoshawishika na kufuata kauli za Mchungaji Gwajima kwani zina lengo la kutishia amani na uchochezi na kwamba kwa kufanya hivyo ni kuleta mifarakano katika jamii pamoja na wananchi na serikali yao na utawala uliopita na wa sasa,” alisema.
Mwenyekiti huyo alimtaka Askofu Gwajima, ajitokeze katika majukwaa ya kisiasa ;na siyo kutumia madhabahu au mimbari kufanya siasa zenye lengo la kuwagawa Watanzania. Ikongo pia alitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuzingatia maelekezo na sheria inazozikabidhi kwa viongozi wa kidini wanaposajili makanisa yao.
No comments:
Post a Comment