Na: Lilian Lundo – MAELEZO.
Zaidi ya Wilaya 81 ambazo zimekuwa hazipati usikivu wa redio ya Taifa nchini kuongezewa usikivu kwa mwaka wa fedha 2016/17 na kuendelea.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,Nape Nnauye(Pichani) leo Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nachingwea Mhe. Hasani Eliasi Masala juu ya kutokusikika redio ya Taifa katika jimbo lake.
Aidha Mhe. Nape amesema kuwa kutosikika kwa redio ya Taifa katika Wilaya hiyo kumetokana na uchakavu wa mitambo, lakini kwa hivi sasa eneo la Nachingwea Mjini linapata matangazo ya redio ya Taifa kwa kutumia mitambo miwili midogo ya Redio-FM ya TBC-FM na mtambo wa TBC-Taifa.
“Nia ya Serikali ni kufunga mitambo mipya na ya kisasa ya FM yenye nguvu kubwa ya kilowati 2 ambao utakuwa na uwezo wa kurusha matangazo yatakayowafikia wananchi sehemu mbali mbali nchi nzima,” alifafanua Mhe. Nape.
Aliendelea kwa kusema kuwa, tathmini iliyofanyika kubaini usikivu wa redio ya Taifa nchini umeonyesha kuwa jumla ya wilaya 81 hazina usikivu mzuri wa redio ya Taifa kutokana na uchakavu wa mitambo.
Aidha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imejipanga kufunga mitambo mipya, sambamba na ukarabati wa majengo ya mitambo, ofisi na miundo mbinu mbalimbali kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017 na kuendelea kwa kuanza na Mikoa iliyopo pembezoni ili kuboresha usikivu ikiwezekana isikike mpaka nchi jirani.
No comments:
Post a Comment