Uongozi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) umekabidhi msaada ya uzio wa waya aina ya seng’enge kwa shule ya sekondari Kisimiri iliyopo Ngarenanyuki wilayani Arumeru mkoa wa Arusha ili kusaidia kuimarisha usalama katika shule hiyo.
Akikabidhi msaada huo jana kwa niaba ya uongozi wa AICC, Afisa Itifaki na Uhusiano wa Kituo hicho, Rodney Thadeus alisema kwamba msaada huo ni mahsusi kwa ajili ya kuweka uzio na kuimarisha usalama wa wanafunzi katika shule hiyo ambayo inapakana na hifadhi ya Taifa ya wanyama ya Arusha.
“Ukiiangalia shule hii utaona ipo pembezoni mwa mbuga ya wanyama, sasa hii ni changamoto ya kiusalama na ndio sababu uongozi wa AICC ukaona usaidie kutatua changamoto hii kwa kutoa mabando 50 ya seng’enge”, alieleza Rodney.
Alieleza kuwa AICC inaamini kuwa mbali na kuimarisha ulinzi, uwepo wa uzio pia utawafanya wanafunzi wabaki katika eneo la shule na kutumia muda wao mwingi kujisomea na hivyo kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Kisimiri Emmanuel Kisongo aliushukuru uongozi wa AICC kwa kuwa taasisi ya kwanza kuitikia wito wa kujenga uzio katika shule hiyo.
“Napenda kuishukuru kwa dhati AICC kwa msaada huu kwani shule hii imepakana na mbuga ya wanyama na wakati mwingine nyakati za usiku fisi, chui na wanyama wengine wanakatisha hapa shuleni na hivyo kuhatarisha usalama wa wanafunzi na walimu wa shule yetu”, alisisitiza Kisongo.
Alieleza kuwa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa uzio liliwekwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na hivyo kuziomba taasisi na wadau mbalimbali kujitokeza kusadia kukamilisha ujenzi wa uzio katika shule hiyo.
Afisa Itifaki na Uhusiano wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC), Rodney Thadeus (kushoto) akimkabidhi bando la sengénge Mwalimu Mkuu wa Shule ya sekondari Kisimiri, Emmanuel Kisongo. AICC amekabidhi mabando 50 ya sengénge kwa ajili ya ujenzi wa uzio ili kuimarisha usalama katika shule hiyo. (Picha kwa hisani ya AICC).
Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Kisimiri iliyopo Ngarenanyuki wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha wakishusha mabando ya sengénge iliyotolewa msaada na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) kwa ajili ya ujenzi wa uzio ili kuimarisha usalama katika shule hiyo. (Picha kwa hisani ya AICC).
No comments:
Post a Comment