ANASWA AKITAKA KADI YA PIKIPIKI YA ' KIMA CHA DAMU' - PATRICIA-TV.com

Breaking

Share daily activities and have all funs here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Sunday, July 24, 2016

ANASWA AKITAKA KADI YA PIKIPIKI YA ' KIMA CHA DAMU'


WATU wawili wamekufa katika matukio tofauti wilayani Kwimba na Nyamagana, ambapo mtu mmoja amekutwa amekufa kifo cha kutilia shaka baada ya kuporwa pikipiki wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Agustino Senga alisema jana kuwa katika tukio la kwanza, Shabani Haruna(32) mwendesha bodaboda na mkazi wa Maliza, Kata ya Buhongwa wilaya ya Nyamagana, alikutwa amekufa akiwa ameporwa pikipiki ambayo namba zake za usajili zilikuwa zimeondolewa.

Alisema tukio hilo lilitokea Julai 20 mwaka huu majira ya saa mbili asubuhi waliukuta mwili wa marehemu umefungwa kamba shingoni na majeraha, hali iliyoashiria alipigwa na kitu kizito.

Kamanda Senga alisema Haruna aliondoka nyumbani kwake Julai 17 mwaka huu kwenda kwenye shughuli zake na hakurudi nyumbani siku hiyo.

“ Ilipofika siku ya Jumatatu, majira ya saa moja na nusu jioni, mke wa marehemu Hamda Issa alitoa taarifa ya kupotea kwa mumewe kwenye kituo cha polisi,” alisema.

“Baada ya kutolewa taarifa ile, tuliweka mtego nyumbani kwa marehemu, ndipo alipokuja kijana mmoja, Metusela Robert (17) mkazi wa Buhongwa akidai kuwa ameagizwa kwenda nyumbani kwa marehemu kuchukua kadi ya usajili wa pikipiki, ndipo alipokamatwa na polisi na kuwekwa chini ya ulinzi,” aliongeza.

Alisema polisi wanaendesha msako wa kuwatafuta watu wengine waliohusika na mauaji hayo na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando kwa ajili ya uchunguzi.

“Natoa mwito kwa wakazi wa mkoa wa Mwanza watoe taarifa mapema kwa jeshi la polisi wakati wanapoona uhalifu unafanyika mahali fulani ili wahalifu waweze kukamatwa,” alisema.

Katika tukio la pili, Anne Martin (18) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Matara, wilaya ya Kwimba, mkoa wa Mwanza alikufa baada ya kuchomwa sindano ya kutoa ujauzito wa miezi mitatu na muuzaji wa duka la dawa baridi, Stephen Ng’wanyi ambaye pia ni mkazi wa Matara.

Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 19 mwaka huu majira ya usiku, ambapo Anne alijisikia kuumwa na tumbo na siku iliyofuata alizidiwa na maumivu ya tumbo.

“Baada ya kuzidiwa na maumivu ya tumbo, alimueleza ukweli dada yake aliyekuwa anaishi naye Anna Fabian kuwa alikuwa na ujauzito wa miezi mitatu na kwamba alichomwa sindano na Stephen Ng’wanyi ili aharibu ujauzito wake,” alifafanua.

Alisema baada ya hali yake kuwa mbaya, dada yake alienda kwa Ng’wanyi ili aende nyumbani kwao ampatie matibabu kwa ajili ya kutibu maumivu ya tumbo.

“ Ng’wanyi alimchukua mgonjwa ili kwenda kumtibu nyumbani, lakini mgonjwa alifariki ndani ya muda mfupi baada ya mtu huyo kutoa taarifa ya kifo, alitoweka kwenda kusikojulikana, ” alisema na kuongeza kuwa polisi inaendelea na msako ili kuhakikisha mtuhumiwa anakamatwa na upelelezi kwa ajili ya kifo hicho unaendelea. “Natoa mwito kwa wanawake na wasichana wasijihusishe kwenye vitendo vya kutoa mimba bila sababu za kitabibu, kwani mwanamke atakayekuwa amefanya hivyo, atakuwa ametenda kosa la jinai,” alisema na kuwataka wamiliki wa maduka ya dawa kufanya biashara hiyo kwa mujibu wa sheria na taaluma zao na si vinginevyo.

Katika tukio la tatu, Kamanda Senga alisema kuwa Elisha Lameck (18), mkazi wa Kitangiri alikutwa akiwa kwenye jaribio la kumbaka mtoto mdogo wa kike (5) nyumbani kwao jina lake linahifadhiwa kwa sababu za kiusalama.

Alisema tukio hilo lilitokea Julai 13 mwaka huu majira ya saa 10.00 jioni katika Mtaa wa Kitangiri, Manispaa ya Ilemela, Mkoa wa Mwanza ambapo mtuhumiwa alifika nyumbani kwa mtoto huyo kwa lengo la kuwasalimia na kumkuta msichana wa kazi aitwaye Zulekha Sameer na mtoto huyo.

“Alimchukua mtoto huyo na kuingia naye chumbani na kufunga mlango, msichana wa kazi alikwenda kuchungulia dirishani na kumuona mtuhumiwa akiwa amevua nguo zake zote pamoja na za mtoto huku akichezea sehemu zake za siri na ndipo alipopiga kelele kuita majirani,” alifafanua.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here