MUHONGO AZIDI KUIBANA TANESCO. - PATRICIA-TV.com

Breaking

Share daily activities and have all funs here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Monday, July 4, 2016

MUHONGO AZIDI KUIBANA TANESCO.


WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameitaka Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha kunakuwa na umeme wa uhakika nchi nzima pamoja na kupima utendaji kazi wa mameneja wa shirika hilo wa ngazi ya wilaya, mkoa na kanda.

Aliyasema hayo jana baada ya kufanya mazungumzo na Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco pamoja na Menejimenti ya Tanesco katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam katika ofisi za Tanesco ikiwa ni mara ya kwanza kwa Profesa Muhongo kufanya kikao na Bodi hiyo tangu ilipozinduliwa Mei mwaka huu.

Muhongo ametaka ifikapo Agosti 30 mwaka huu vitu vyote vya zamani vya shirika hilo viwe vimekamilika na kuanza na mambo mapya, ikiwa ni pamoja na mikataba mbalimbali na kutoa vipaumbele vya kazi ili nchi iwe na umeme wa uhakika utakaotosheleza mahitaji ya wananchi.

Kuhusu majadiliano ya mikataba mbalimbali, Profesa Muhongo aliitaka Bodi hiyo kuhakikisha kuwa majadiliano hayo yanapangiwa muda maalumu wa kumalizika bila kuchukua muda mrefu.

“Ifike mahala kampuni au mtu aambiwe kama mkataba husika unawezekana au hauwezekani badala ya kuwa na majadiliano ya muda mrefu yasiyokuwa na ukomo, hivyo mikataba ambayo haijakamilika, Menejimenti iiwasilishe kwa Bodi. Tunataka ifikapo Agosti 30, 2016 vitu vyote vya zamani viwe vimekamilika ili tuanze masuala mapya,” alisema Profesa Muhongo.

Profesa Muhongo aliitaka Bodi hiyo kuhakikisha kuwa kunakuwa na upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme ikiwemo ya upanuzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi I, kiasi cha megawati 185 na ujenzi wa mradi wa Kinyerezi II wa megawati 240.

Ameitaka Bodi hiyo kujituma na kukutana kila baada ya miezi mitatu ili kutathmini mapato ya shirika ikiwa ni pamoja na kupima utendaji kazi wa mameneja wa Tanesco katika ngazi ya wilaya, mkoa na kanda.

Alisema mameneja hao watapimwa kwa kutumia vigezo vitatu ambavyo ni kuongeza makusanyo ya mapato, kuongeza idadi ya wateja wapya waliounganishwa na huduma ya umeme na ubunifu wa kutatua matatizo ya umeme katika maeneo wanayoyasimamia.

“Mfano unakuta nguzo za umeme zinaoza hadi zinaanguka chini na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa wakati kuna meneja katika eneo hilo la kazi, hii haikubaliki,” alisema Profesa Muhongo.

Muhongo alisisitiza kuwa changamoto zilizopo za upatikanaji wa umeme wa uhakika na usambazaji wa nishati hiyo zisimamiwe kwa umakini ili ziweze kutatuliwa ndani ya miaka mitatu.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe alisema bado kuna jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa umeme unawafikia wananchi wengi, hivyo alihimiza Tanesco kufanya kazi kwa ufanisi ili izalishe umeme mwingi na kusambaza kwa wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Dk Alex Kyaruzi, alisema bodi hiyo ina uwezo wa kufanyia kazi maagizo yaliyotolewa na Profesa Muhongo na kuahidi kuwa watayatekeleza na kusimamia kwa umakini Menejimenti ili ifanye kazi kwa ufanisi unaotakiwa

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here