Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia wafanyabiashara wa Rwanda kuwa bandari ya Dar es salaam ni salama kwa wao kupitisha mizigo na ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua za kuiboresha bandari hiyo na kurahisisha biashara kati ya nchi hizi mbili.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 01 Julai, 2016 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Tanzania na Rwanda kupitia vyombo vya habari wakati wa ziara rasmi ya kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame inayofanyika kwa siku mbili hapa nchini.
Dkt. Magufuli amesema pamoja na kuchukua hatua kadhaa za kuboresha bandari ya Dar es salaam kwa manufaa ya wafanyabiashara wanaopitisha mizigo, Tanzania imeamua kuipatia Rwanda eneo la kujenga bandari kavu kwa ajili ya mizigo ya wafanyabiashara wake na pia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) itafungua ofisi Mjini Kigali nchini Rwanda ikiwa ni juhudi za kurahisisha na kuongeza biashara kati ya nchi hizi mbili.
Aidha, Rais Magufuli amesema kwa kutambua umuhimu wa reli ya kati kwa uchumi wa Tanzania na Rwanda, Tanzania imetenga shilingi Trilioni moja katika bajeti mpya ya serikali kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Reli hiyo kwa kiwango cha kisasa yaani “Standard Gauge” na kwamba ni matarajio kuwa wadau wengine wa maendeleo watajitokeza kuunga mkono juhudi za ujenzi wa reli hiyo hapa Tanzania na nchini Rwanda huku akidokeza kuwa China imeonesha nia ya kuunga mkono mradi huo.
Dkt. Magufuli ameongeza kuwa serikali yake pia imechukua hatua madhubuti za kulifufua shirika la ndege la Taifa na kwamba tayari mipango imefanywa kuhakikisha ndege mbili aina Bombadier Q400 zinanunuliwa na zitatua hapa nchini kabla ya mwisho wa mwezi Septemba Mwaka huu 2016.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame amemshukuru Rais Magufuli kwa kumualika kufanya ziara rasmi ya kiserikali hapa nchini na amemhakikishia kuwa serikali yake itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo kati ya nchi yake na Tanzania kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.
Majira ya jioni Rais Kagame akiwa na mwenyeji wake Rais Magufuli, amefungua rasmi maonesho ya 40 ya kimataifa ya Biashara Dar es salaam yanayofanyika katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo Barabara ya Kilwa, Wilaya ya Temeke, Mkoani Dar es salaam.
Akizungumza kabla ya kuzindua rasmi maonesho hayo, Rais Kagame ametoa wito kwa Tanzania na Rwanda pamoja na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki kushirikiana na sekta binafsi katika kutumia fursa nyingi za kibiashara zilizopo baina yake na kuwaletea manufaa wananchi.
Nae Rais Magufuli amezipongeza nchi takribani 30 zilizojitokeza kushiriki katika maadhimisho hayo zikiwemo kampuni zaidi ya 650 na wadau zaidi ya 2,000 na amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zenye watu takribani milioni 165 na nchi nyingine za Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) kuongeza biashara baina yake kwa kuwa hivi sasa kiwango cha biashara baina ya nchi hizo ni cha chini mno.
Baada ya kufungua maonesho hayo, Rais Kagame na mwenyeji wake Rais Magufuli wametembelea mabanda mbalimbali ya maonesho ya bidhaa na huduma katika viwanja vya Sabasaba na baadaye Rais Kagame atahudhuria dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na mwenyekiji wake Rais John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
01 Julai, 2016
No comments:
Post a Comment