* Waliopotelewa wajisalimisha NECTA, matangazo kwenye magazeti sasa yafurika
* NSSF yagoma kulipa ambao hawajawasilisha vyeti halisi
Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
IDADI ya matangazo ya watu waliopotelewa na vyeti vyao halisi vya kidato cha nne na sita katika vyombo mbalimbali vya habari, hususani magazeti imeongezeka na hivyo kujenga hisia kwamba hatua hiyo imetokana na agizo la Serikali kutaka kila mtumishi wake kuhakikiwa vyeti vyake halisi.
Mbali na matangazo, uchunguzi wa gazeti hili pia umebaini kuwapo kwa idadi kubwa ya watu wanaofika Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kwa ajili ya kufuatilia vyeti vyao hivyo.
Vyeti hivyo ambavyo hutolewa na NECTA baada ya mtahiniwa kuhitimu mtihani wake, kwa kawaida inapotokea mtu amepotelewa hutakiwa kutoa taarifa kituo cha polisi, kisha kutoa tangazo kwa umma kupitia vyombo vya habari, hususani magazeti.
Katika uchunguzi wake huo, MTANZANIA Jumamosi limebaini kuwa tangu Serikali itoe agizo hilo, kwa siku katika magazeti matano kuna wastani wa matangazo 50. Hali hiyo ni tofauti na siku za nyuma ambapo matangazo kama hayo ni nadra kukutana nayo.
Kwa muktadha huo huo, gazeti hili lilifika katika ofisi za Necta zilizoko eneo la Bamaga, Mwenge na kukuta vijana na watu wazima takribani 30 waliokuwa wakijaza fomu mbalimbali za kuomba vyeti.
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa vijana hao ambaye hata hivyo hakutaka jina lake litajwe gazetini, alikiri kuwa amepotelewa na cheti chake cha awali na alikuwa amefika hapo kwa ajili ya kuomba.
“Acha tu dada, yaani hata kilipopotelea sijui, kwa hiyo imebidi nifuate utaratibu wa kuomba tena,” alisema kijana huyo. Wakati gazeti hili likiondoka katika ofisi hizo lilikutana na kijana mwingine aliyejitambulisha kwa jina la John Kimario, ambaye naye alikuwa akitaka kujua zilipo ofisi za Necta akiwa na tatizo kama hilo.
“Nilipoteza vyeti vyangu, sasa nimeelekezwa kushuka Bamaga ila sijui zilipo ofisi hizo,” aliuliza na kisha mwandishi wa habari hizi kumuonyesha ofisi za Necta zilipo.
Hivi karibuni Serikali Kuu pamoja na taasisi zake zilitoa agizo la kutaka kila mtumishi wake kuhakikiwa vyeti vyake halisi. Uamuzi huo pamoja na mambo mengine, umelenga kuwaondoa watumishi wasio na sifa pamoja wale hewa ambao inadaiwa walikuwa wakiibia Serikali na kuwabakisha walio halali ambao wanastahili kulipwa mishahara.
Tangazo la NSSF
Katika tangazo lake la Julai 19, mwaka huu, Shirika hilo lilitangaza kusitisha mishahara ya wafanyakazi wake watakaoshindwa kuwasilisha vyeti halisi vya taaluma zao.
Hiyo ilikuwa ni siku chache baada ya Shirika hilo kuwasimamisha wakurugenzi wake sita, mameneja watano na mhasibu mkuu kwa tuhuma mbalimbali za ubadhirifu.
Tangazo hilo lililosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara, lilieleza kuwa uamuzi huo umefikiwa kutokana na baadhi ya wafanyakazi kushindwa kuwasilisha vyeti hivyo kama ambavyo waliagizwa kufanya hivyo kabla ya Juni 24, mwaka huu.
“Kutokana na hali hiyo, Shirika halitalipa mishahara wafanyakazi hao hadi watakapowasilisha vyeti vyao kwa wakuu wa idara na mameneja wa kanda kama agizo la serikali lilivyowataka.
“Nawajulisha kuwa wote walioshindwa kuwasilisha vyeti halali hawatalipwa mishahara yao hadi watakapowasilisha vyeti hivyo kama ilivyoelekezwa,” alisisitiza Mkurugenzi huyo katika barua yake hiyo kwa wakuu wa idara za ofisi hiyo.
Pwani kwafukuta
Hatua hiyo ya uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma mkoani Pwani nako kumewaweka watumishi wapatao 3,600 kwenye hatari ya kukosa mishahara ya Agosti, mwaka huu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angela Kairuki, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema hiyo inatokana na kubainika kwa mapungufu katika taarifa zao.
Alisema kati ya hao, watumishi 3,569 taarifa zao za kielimu hazionekani, 36 wana zaidi ya miaka 60 lakini wako kazini badala ya kuwa wamestaafu, sita akaunti zao hazitambuliki na 21 vyeo vyao havijabainishwa.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, Bagamoyo wapo watumishi 2,175 wenye taarifa zenye upungufu, Rufiji 912, Kibaha Mji 465, Mkuranga 21, Kibaha Vijijini 14, Mafia na Kisarawe wanane.
“Hivyo haitawezekana kulipwa mishahara kuanzia Agosti hadi hapo mapungufu ya taarifa zao zitakaporekebishwa,” alisema.
Bandari ya Tanga nako
Julai 20 mwaka huu Bandari ya Tanga nayo ilitoa tangazo lililosainiwa na Ofisa Rasilimali Watu Mkuu, I.A Malombe, likiwataka wafanyakazi wote wa bandari hiyo kuwasilisha nakala zao za vyeti halisi.
“Tunapenda kuwataarifu wafanyakazi wote wa bandari kuwa mnatakiwa kuwasilisha vyeti vyenu halisi ‘original’ katika ofisi ya rasilimali watu vikiwa katika bahasha ambazo juu yake ziwe zimeandikwa jina, namba ya kazi ya mfanyakazi husika, cheo alichonacho pamoja na idara anayofanya kazi .
“Vyeti hivyo ni vya elimu ya kidato cha nne, sita na vya taaluma mbalimbali. Zoezi hili linaanza mara moja msomapo tangazo hili, atakayeliona mtaarifu na mwenzake,” linasomeka tangazo hilo.
NECTA
MTANZANIA lilimtafuta Ofisa Habari wa Necta, John Nchimbi, kuhusiana na suala hilo, hata hivyo, jitihada za gazeti hili hazikuzaa matunda kwa kile kilichoelezwa alikuwa na majukumu mengine ya kikazi.
Hata hivyo, Necta imeahidi kukutana na timu ya waandishi wa gazeti hili siku ya Jumanne wiki ijayo ili kulizungumzia suala hilo.
Pamoja na hayo, akitangaza matokeo ya kidato cha sita, Julai 15, mwaka huu, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, aliwataka wanaojijua kuwa wanamiliki vyeti bandia waanze kujisalimisha wao wenyewe, kwani wanao uwezo wa kuwakamata popote pale walipo.
No comments:
Post a Comment