HUZUNI YATAWALA : WAZIRI MKUU AONGOZA WANANCHI KUAGA MIILI YA WALIOKUFA KWA TETEMEKO - PATRICIA-TV.com

Breaking

Share daily activities and have all funs here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Sunday, September 11, 2016

HUZUNI YATAWALA : WAZIRI MKUU AONGOZA WANANCHI KUAGA MIILI YA WALIOKUFA KWA TETEMEKO


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza maelfu ya wananchi wa Manispaa ya Bukoba mjini kuaga miili ya watu 16 waliofariki kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea Jumamosi, 10 Septemba, 2016 mkoani Kagera.

Tetemeko hilo imesababisha vifo vya watu 16 na wengine 253 kujeruhiwa. Pia limesababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.

Kufuatia tukio hilo Waziri Mkuu ambaye alimuwakilisha Mheshimiwa Rais, Dk. John Magufuli amewaomba wananchi kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kufanya tathmini ya athari zilizotokana na maafa hayo.

“Poleni sana tukio hili ni kubwa na halijawahi kutokea nchini. Haya yote ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Tuendelee kuwa na imani na watulivu Serikali ipo pamoja nanyi na haitawatupa mkono,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Kamati ya Maafa ambayo ipo katika Ofisi ya Waziri ya Mkuu itakwenda wilaya za Kyerwa, Karagwe na Bukoba mjini kwa ajili ya kufanya tathmini na kubaini athari zilizosababishwa na tetemeko hilo na kuona namna ya kuwasaidia waathirika.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa mkoa huo kuchukua hatua za haraka kwa kuwatafutia eneo salama la kulala wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyakato ambayo mabweni yake yote yameathirika na tetemeko hilo na hayafai kutumika.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kutembelea shule hiyo na kujionea namna mabweni ya shule hiyo yalivyopata nyufa hali iliyosababisha wanafunzi kulala uwanjani.

Pia Waziri Mkuu ameiagiza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuangalia kama kuna tetemeko lingine linaweza kutokea nchini ili Serikali iweze kuchukua tahadhari pamoja na kutoa elimu kwa umma namna ya kujikinga.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu amesema kwa sasa wanaendelea na jukumu la kuwatafutia makazi wananchi ambao nyumba zao zimeanguka. Pia mkoa unaendelea kufanya tathmini ya kina kujua athari zilizosababishwa na tetemeko hilo.

Awali Waziri Mkuu alitembelea Hospitali ya Mkoa wa Kagera ambako majeruhi 170 wamelazwa na kutoa pole na kwamba anawaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na wenye matatizo ambayo yanahitaji matibabu kwenye hoispitali kubwa Serikali itahakikisha wanapelekwa huko na kuhudumiwa.

IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Pichani kulia ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimuelekeza jambo Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salim Mustafa Kijuu ,kabla ya kuanza sala ya pamoja ya kuwaaga na kutoa heshima za mwisho kwa miili ya marehemu,waliokumbwa na tukio la tetemeko la Ardhi


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimuelekeza jambo Mbunge wa jimbo la BUkoba Mjini,Mh Wilfred Lwakatare,kabla ya kuanza sala ya pamoja ya kuwaaga na kutoa heshima za mwisho kwa miili ya marehemu,waliokumbwa na tukio la tetemeko la Ardhi



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here