Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Etienne Ndayiragije amewaambia Warundi kuwa yupo kazini, hivyo wasitarajie huruma yoyote kutoka kwake.
Ndayiragije ambaye ni raia wa Burundi anatarajiwa kuiongoza Taifa Stars dhidi ya taifa lake la Burundi katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Qatar mwaka 2022.
Ndayiragije alisema kuwa kwa sasa yupo kazini na malengo yake ni kuona jinsi gani atawasaidia waajiri wake ambao ni timu ya Tanzania kupata ushindi.
“Nipo kazini kwa sasa, waajiri wangu ni Watanzania ambao wote kwa pamoja tuna malengo ya kuifanikisha Tanzania kufuzu Kombe la Dunia, Burundi pia wana ndoto hizo hivyo wanatakiwa kupambana kwa ajili ya hilo,” alisema kocha huyo.
Naye kiungo wa Taifa Stars, Himid Mao amesema: “Mechi haitakuwa nyepesi, timu za Afrika Mashariki zinapokutana huwa mchezo unakuwa mgumu kwa kuwa kuna ile hali ya kujuana lakini bado tuna nafasi ya kufanya vizuri. Kila mchezaji kati yetu anajua umuhimu wa mechi ya ugenini na nyumbani pia.”
Tanzania, keshokutwa Jumatano ikiwa ugenini nchini Burundi itacheza mchezo huo wa kwanza wa kufuzu Kombe la Dunia ambapo marudiano yatafanyika Septemba 8 jijini Dar.
Tanzania na Burundi zinacheza mchezo huo kuwa kuwa ni baadhi ya timu mbazo zipo chini katika viwango vya ubora wa soka Afrika, ambapo zinawania kuelekea kucheza katika Hatua ya Makundi ikiwa ni mwendelezo wa kuwania kufuzu.
Mchezo wa keshokutwa utachezwa kwenye Uwanja wa Prince Louis Rwagasore jijini Bujumbura.
No comments:
Post a Comment