MFANYABIASHARA Alex Msama amemuomba radhi Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe kufuatia habari mbili zilizochapishwa katika Gazeti la Dira ya Mtanzania analolimiliki.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Msama alisema amejiridhisha kuwa habari hiyo iliyobeba kichwa cha habari ‘Utapeli wa Mwakyembe wamwagwa hadharani’ haikufuata misingi ya uandishi wa habari.
Habari nyingine ambayo imeonekana kumchafua Dk Mwakyembe ni ile ya Mwakyembe atuhumiwa kutapeli bilioni 2 ambazo zimemuumiza kiongozi huyo.
Alisema yeye kama mmiliki wa gazeti hilo amesikitishwa na habari hiyo na kwamba hatua ya kwanza anayoichukua ni kumuomba radhi Waziri Mwakyembe.
Msama alisema sambamba na kuomba radhi atamfikishia barua Mwakyembe ya kumtaka radhi kwa tukio hilo.
“Nimesikitishwa na habari hii kwa kuwa haikuzingatia misingi ya uandishi wa habari, ilihukumu na kuonyesha kuwa lengo lake lilikuwa kumharibia jina Waziri Mwakyembe, ninachukua nafasi hii kumuomba radhi nikiwa mmiliki wa gazeti hilo,” alisema Msama.
Aidha Msama alisema hatua nyingine anayochukua ni kumsimamisha kazi mhariri wa gazeti hilo, Mussa Mkama kwa kuwa alishindwa kufanya kazi yake kwa umakini ya kuhakikisha habari anazozipitisha zinafuata misingi ya uandishi wa habari na weledi.
Alisema Mkama alipaswa kuhakikisha anafuata weledi lakini alishindwa kufanya hivyo kwa hiyo anamsimamisha kazi na kwamba hatua nyingine kali za kinidhamu zitafuata.
“Mimi ni mfanyabiashara sijui mambo ya uandishi, nilimuajiri nikiamini atasimamia yale aliyofundishwa chuoni, kwa kuwa ameshindwa inabidi akae pembeni kwanza,” alisisitiza Msama.
Ameahidi kuwa katika Gazeti la Dira ya Mtanzania litakalotoka Juni 27, kwa ukubwa uleule atamuomba radhi Waziri Mwakyembe.
Hivi karibuni Waziri Mwakyembe aliitisha mkutano wa waandishi wa habari mjini Dodoma akilalamikia kuwa habari mbili za gazeti hilo iliyochapishwa na Gazeti la Dira ya Mtanzania la Juni 20 na la Juni 23 mwaka huu zililenga kumchafua na kuahidi kuwa atalishtaki kupitia habari hizo mbili.
No comments:
Post a Comment