Kauli ya Rais ya Kuzuia Vyama vya Siasa Kufanya Shughuli za Siasa kwa Miaka Mitano ni Tangazo la Vita dhidi ya Demokrasia na Mfumo wa Vyama vingi Nchini
Tumepokea kwa MSHTUKO na masikitiko makubwa kauli ya Rais kwamba vyama vya siasa havipaswi kufanya siasa isipokuwa wakati wa Kampeni na kupitia bungeni.
Kimsingi kauli ya Rais ni kauli yenye nia ya kuvunja Sheria ya Vyama vya siasa inayolinda uwepo wa mfumo wa vyama vingi na kuhimiza vyaMA vya siasa kufanya shughuli za siasa katika msimu wote ili kuthibitisha uhai wao.
Tunaichukulia kauli ya Rais kama tangazo la vita dhidi ya demokrasia na uhai wa vyama vingi nchini. Chama chetu kitaitisha vikao vya dharura kujadili hali ya siasa nchini na namna ya kukabiliana na mashambulizi yanayoendelea dhidi ya demokrasia nchini mwetu.
Tunatoa wito kwa vyama vyote vya siasa vinavyoamini katika misingi ya demokrasia nchini kukutana haraka na kujadili namna ya kuunganisha nguvu pamoja katika kupigana vita mpya ya kulinda demokrasia nchini mwetu.
Aidha, tunatoa wito kwa wananchi wote na taasisi za kiraia kusimama imara katika kulinda demokrasia. Tunasisitiza kuwa ushahidi wa kisayansi duniani kote unaonyesha kuwa huwezi kuua demokrasia bila kuua juhudi za maendeleo. Tusiruhusu mtu yeyote mwenye mamlaka kuua demokrasia nchini mwetu.
Hatua zozote za kuua demokrasia ni kuua Umoja, Amani na Mshikamano wa wananchi na Taifa, ambayo ndiyo misingi ya maendeleo ya nchi yetu kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Tunatoa wito kwa wananchi wote kushikamana na kusimama imara katika kipindi hiki kigumu ili kulinda demokrasia.
Zitto Kabwe, MB
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Alhamisi, 23 Juni 2016.
No comments:
Post a Comment