Mwezi huu ni wa baraka sana kwa mashabiki wa mpira dunia nzima, kwani tumeweza kupata bahati ya kushudia michuano ya Copa Amerika Centenario na Euro 2016 ikipigika kwa wakati mmoja. Michuano ya Copa Amerika na Euro yote hufanyika baada ya miaka minne na unaweza kushangaa inakuwaje kwamba Copa Amerika inachezwa tena mwaka huu wakati Chile ilitoka kutwaa ubingwa huo mwaka jana tu. Hii ni kwa sababu michuano ya mwaka huu si ya kawaida bali imeandaliwa kuadhimisha miaka 100 ya michuano ya Copa Amerika.
Zikiwa zimeshapigika mechi kadhaa katika michuano hii yote, hakika hivi sasa tuko kwenye nafasi nzuri ya kuweza kutoa maoni juu ya mashindano haya.
Mpaka sasa hivi inaonekana kwamba Michuano ya Copa Amerika ndiyo yenye msisimko zaidi kufuatilia ukilinganisha na Michuano ya Euro kwani mwaka huu timu za Euro zimekuja na style ya kukaba sana na kunyimana nafasi huku kila timu ikimuogopa mwenzake.
Magoli yamekuwa adimu sana kupatikana, hakika hii inachangiwa na muundo mpya wa michuano ya Euro ya timu ya 24, kitu ambacho kimefanya timu ndogondogo kupata nafasi ya kushiriki kwenye michuano hii. Timu hizi hutegemea kukaba kuanzia dakika ya kwanza mpaka dakika ya mwisho ili kupata matokeo wanayotaka.
Hakika hata nyota wa Ureno Ronaldo alishaliona hili na baada ya mechi na Iceland iliyoisha kwa droo ya 1-1 alisema “Iceland hawakujaribu chochote, wao ilikuja kukaba tu na kutegema Counter attack…walivyoshangilia kule mwishoni nilidhani wameshinda Euro yenyewe sikuamini. Wanapocheza mpira kwa kukaba hii ianonesha kwamba bado wana fikra za timu ndogo na hawatofanya chochote kwenye michuano hii.”
Zamani michuano ya Euro ilikuwa ina timu 16 na vumbi lilikuwa linaanza kutimuliwa kuanzia filimbi ya kwanza ya mechi ya kwanza, hii ni kwa sababu timu hizi 16 zote zinazoingia huwa na uwezo mkubwa tena ambao haupishani sana, na kupata droo katika kundi lenye mechi tatu tu kilikuwa ni kitu ambacho hakikuwa na msaada sana.
Mfumo mpya huu wa sasa wa Euro ambapo hata timu inayomaliza nafasi ya tatu inaweza kufuzu kwenda kwenye hatua nyingine, umesaidia kuongeza mpira wa kukaba sana kwani hata hiyo pointi moja inaweza kukusaidia kufuzu kwenda kwenye hatua nyingine.
Kuna takwimu moja niliiona ikanishangaza sana takwimu hii ilisema kwamba endapo mechi kati ya Belgium na Ireland ingeisha 0-0 na timu ya Ireland ingechapwa 2-0 na Italy na mechi kati ya Italy na Sweden iishe kwa droo ya 0-0 basi timu ya Sweden ikiongozwa na Zlatan Ibrahimovic ingeweza kufuzu kwenda hatua ya mtoano ikiwa haijapiga shuti hata moja golini.
Japo mpira wa kukaba sana umeanza kupungua katika mechi za karibuni, lakini hakika kwa sasa hivi Copa Amerika ndiyo yenye msisimko zaidi. Kwa upande wa Copa Amerika huku karibia kila mechi ni mvua ya magoli.
Huku mpaka sasa hivi zimejitokeza stori kibao za kufurahisha kama vile Messi kupiga Hat trick ndani ya dakika 19 tena akiwa majeruhi, timu ya Uruguay ikiongozwa na Suarez na Cavani na timu ya Brazil kutolewa kwenye mashindano haya hatua ya makundi, timu ya Marekani kufika nusu fainali ya michuano hii na nyinginezo kibao.
Na hata siku ya juzi ilijitokeza stori nyingine kali baada ya timu ya Chile kuitwanga Mexico ambayo chini ya kocha wao mpya Osario iliweza kushinda mechi 11 mfululizo 7-0 tena mbele ya mashabiki 70,000 wengi wao wakiwa wamexico. Eduardo Vargas kama ilivyokuwa kawaida yake avaapo uzi wa nchi ya Chile alitupia goli nne kwenye hii mechi huku Sanchez akifunga moja na kutengeneza mengine mawili.
Hii haikuwa mara ya kwanza kwa timu kushinda kwa goli 7 kwenye michuano hii kwani siku kadhaa kabla Brazil naye alitoka kushinda kwa idadi hiyohiyo dhidi ya Peru. Chakushangaza ni kwamba, Brazil huyuhuyu aliaga mashindano hayo siku kadhaa zilizofuata baada ya kukubali kichapo kwa Peru.
Labda hali hii inachangiwa na utamaduni tofauti kwenye mpira baina ya mabara haya mawili, bara la America ya Kusini mpira wa kukaba unapigwa vita sana na si kitu cha ajabu kusikia kama kocha amefukuzwa kazi kwa sababu ya mpira wa kukaba hata kama timu yake inashinda. Kocha wa Brazil aliachishwa kazi kwa mara ya pili wiki hii kwa sababu ya ubutu wa timu yake golini kwenye mechi kadhaa uliofanya Brazil waage mashindano mapema.
Mpira wa Amerika ya Kusini na Kati ni wa kasi sana, unaotumia mbinu chache na kukaba hakutiliwi maanani sana ukiangalia takwimu mpaka sasa hivi utagundua kwamba kila mechi ya Copa Amerika huzalisha karibia goli nne kwa mechi wakati kwa Euro ni chini ya Goli mbili kwa mechi
Lakini Bado ni mapema sana na hakika mambo yatachangamka kadri muda unavyozidi kwenda kwani hata washambuliaji tegemezi ambao walitabiriwa kufanya makubwa kwenye michuano ya Euro kama Lukaku na Morata wameaanza tena konesha dalili kwamba wanakumbuka goli liko wapi na wakiendelea kufanya hivyo basi tukae chonjo kusubiria hatua ya mtoano itayokuwa na msisimko zaidi.
No comments:
Post a Comment