JK ; MNYONGE MNYONGENI HAKI YAKE MPENI. - PATRICIA-TV.com

Breaking

Share daily activities and have all funs here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Monday, June 20, 2016

JK ; MNYONGE MNYONGENI HAKI YAKE MPENI.


DAR ES SALAAM: Siku chache kufuatia Kituo cha Ufundi cha Kilimo na Maendeleo Vijijini (Technical Centre for Agricultural and Rural Cooperation, CTA) kilicho chini ya Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) chenye makao makuu Wageningen, Uholanzi kumteua Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete kuwa Balozi wa Heshima (Goodwill Ambassador) wa Maendeleo ya Kilimo barani Afrika, Karibiani na Pasifiki, Wabongo nao wametoa neno.

CTA wamemteua Dk. Kikwete ‘JK’ ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, kwa kutambua mchango na juhudi zake katika kukiendeleza kilimo nchini Tanzania na barani Afrika.

Wakizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar, baadhi ya wasomaji walisema kuwa, wamefarijika kusikia JK amelamba shavu hilo na kuongeza kuwa, Wabongo wazingatie ule msemo wa ‘Mnyonge Mnyongeni Haki Yake Mpeni’.

Walisema kuwa, JK ameondoka madarakani mwaka jana (2015) huku baadhi ya watu wakianza kusema hajafanya kitu lakini wamesahau kuwa, historia ya nchi inaonesha kila rais alipomaliza muda wake, alifanya makubwa kwa taifa.

“Mimi nimefarijika kusikia JK kapewa ubalozi wa heshima. Wenzetu nje wameona hivyo, sisi tunataka kuleta manenomaneno, eti JK hajafanya kitu.


“Hali ya barabara nzuri zilizopo nchini kwa sasa, kuwepo kwa madaraja makubwa kama Kigamboni, hizi barabara za juu (flyover) zilizowekewa jiwe la msingi hivi karibuni, Chuo Kikuu cha Dodoma ‘Udom’ ni kazi za JK.

“Lakini watu wamesahau kabisa na kusema hajafanya lolote. Hivi ni kweli kabisa Watanzania tumefikia hatua
ya kukosa shukurani kiasi hiki?!

Leo hii, Rais John Magufuli ameanza vizuri kabisa, lakini kwa Wabongo, akimaliza si ajabu kusikia hakufanya lolote,” alisema Anthony Chiluba, mkazi wa Mabibo, Dar.

Shukuru Jumbe, mkazi wa Kimara-Kibo, Dar yeye alisema: “Mimi naamini katika utawala wa JK alifanya makubwa kama anavyofanya sasa Magufuli naye kwa nafasi yake.

“Ukiachilia mbali Magufuli kuingia na Mahakama ya Mafisadi, tunampongeza sana lakini JK ndiye rais aliyewaacha viongozi wake wa ngazi za juu wengi kusimama kortini na kufungwa licha ya kwamba alikuwa anaweza kutia mkono wakawa huru au wasishitakiwe kabisa.

“Mfano, aliwaacha Daniel Yona (aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini), Basil Mramba (aliyekuwa Waziri wa Fedha), wakashi takiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi, wakapatikana na hatia, wakafungwa.

“Lakini pia, JK aliwaacha wapande kizimbani aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Constantine Mahalu (aliachiwa huru na korti), aliyekuwa Mkurugenzi wa Tanesco, William Mhando (aliachiwa huru na korti), aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Abdallah Zombe (aliachiwa huru).

“Pia aliachia wapande kizimbani, aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Benki Kuu, marehemu Amatus Liyumba (alifugwa) na aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Ndege, David Mataka (kesi inaendelea). Angekuwa hakufanya kitu, hao vigogo wote wangepeta tu.

“JK amejenga madaraja karibu kumi na mbili nchini kote. Madaraja 12, kuna lile la Rusumo (Kagera), Umoja (Mtwara), Mwanhuzi (Simiyu), Kikwete (Kigoma), Nangoo (Mtwara), Ruhekei (Ruvuma), Mbutu (Tabora), Mwatisi (Morogoro), Ruvu (Pwani), Nanganga (Mtwara), Maligisu (Mwanza) na daraja la waenda kwa miguu la Mabatini (Mwanza),” alisema Shukuru.

Kwa ujumla, wasomaji wengi walionesha hisia zao na msemo wa ‘mnyonge mnyongeni’ wakitoa wito kwa Wabongo kujenga tabia ya kushukuru pia badala ya kuangalia mabaya peke yake.

Katika wadhifa wake huo mpya, CTA imemuomba JK kuiwakilisha katika makongamano ya kimataifa ambapo atazungumzia umuhimu wa kuendeleza kilimo kwa ajili ya kutoa fursa ya ajira zenye staha na uhakika kwa vijana na wanawake katika nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki.

JK amekubali uteuzi huo na kuahidi kushirikiana na CTA katika kutekeleza mambo ambayo ameombwa kusaidiana na taasisi hiyo ambayo ni ya ushirikiano wa Umoja wa Ulaya na Kundi la nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki wenye makao makuu mjini Brussels nchini Ubelgiji.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here