Wakati Kamati ya Haki, Maadili na Madara ya Bunge imepokea mashtaka dhidi ya Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, mbunge mwingine wa upinzani ameamua kumshtaki kiongozi huyo kwenye Kamati ya Kanuni ya Bunge.
Mbunge wa kwanza kumshtaki Dk Tulia, alikuwa Mbunge wa Simanjiro (Chadema), James ole Millya aliyewasilisha kusudio lake kwa Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai mashtaka sita na tayari yamewasilishwa kwenye kamati husika.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alitangaza jana uamuzi wake wa kumshtaki Dk Tulia, ambaye ndiye anayeliongoza Bunge kwa sasa.
Dk Tulia atakuwa na kesi mbili, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka na kwenye Kamati ya Kanuni.
Dk Tulia anakuwa Naibu Spika wa kwanza tangu kuanza Bunge linalojumuisha wabunge wa upinzani, kushtakiwa kwa madai ya kukiuka kanuni na taratibu za Bunge.
Kubenea alisema ameamua kumshtaki Dk Tulia katika kamati hiyo akidai kuwa alivunja kanuni na taratibu wakati akiwasilisha malalamiko ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwa mbunge huyo alisema uongo bungeni.
Akizungumza na wanahabari, mbunge huyo alisema hakuridhishwa na hatua ya Dk Tulia aliyoifanya Mei 13 na kwamba tayari alishawasilisha barua yake yenye hoja tano za mapungufu ya kikanuni kwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah tangu Ijumaa iliyopita.
Kubenea alieleza kuwa Dk Tulia alitumia kanuni ya 71 kupokea malalamiko ya Dk Mwinyi kinyume na utaratibu kwa kuwa kanuni hiyo huruhusu watu wasio wabunge kupeleka malalamiko yao kwa Spika, iwapo masuala yaliyojadiliwa bungeni yamewaathiri.
Alisema wakati akichangia hoja ya wizara hiyo Mei 10, alimtaka Dk Mwinyi aeleze juu ya kuwapo kwa mkataba baina ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Kampuni ya Heinan Guoji Industry & Investment Limited na kama upo haoni kama kuna mgongano wa masilahi kutokana na kushiriki kumjengea nyumba yake.
Hata hivyo, alidai hakuna mbunge aliyesimama kudai hoja hiyo ilikuwa ya uongo kama kanuni ya 63(3) inavyotaka, badala yake siku tatu baadaye alitakiwa kufuta bungeni jambo ambalo anaona Dk Tulia hakumtendea haki.
“Naibu Spika wakati akitoa mwongozo wa Spika alinukuu sehemu tu ya maelezo yangu jambo lilipotosha misingi na mantiki ya mchango wangu bungeni hivyo kuashiria alikuwa na nia mbaya dhidi yangu,” alisema Kubenea na kuongeza: “Hata nilipoomba kufanya hivyo siku aliposoma mwongozo na kunipa nafasi ya kufuta maneno yangu au kuyathibitisha, alikataa na endapo angezingatia mchango wangu wote angetenda haki.”
Katika barua hiyo, Kubenea amelalamika kuwa wakati Dk Tulia anapokea malalamiko kutoka kwa Dk Mwinyi hakumpelekea nakala ili kurahisisha utetezi wake.
Pia, alieleza kuwa Naibu Spika aliamua kimakosa kuwasilisha tuhuma dhidi yake kwenye kamati hiyo bila kuzingatia maelezo aliyowasilisha kwake na vielelezo huku akijua Waziri huyo wa ulinzi alikiuka kanuni ya 63 (3) na 64(2).
Kubenea alisema anaiomba Kamati ya Kanuni yenye nguvu kuliko Spika kusimamisha mchakato unaoendelea kufanywa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge juu ya suala lake hadi pale itakapofanya uamuzi iwapo ilifuata kanuni ama la.
Katika barua hiyo, Kubenea anamuomba Dk Kashililah amjulishe Spika ili aweze kuitisha kikao cha Kamati ya Kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 5(5) ili kuona kama kulikuwa na uhalali wa shauri lake na anaamini Katibu huyo wa Bunge atamtendea haki.
Kubenea alishahojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Alhamisi iliyopita na kueleza kuwa alikubali kufanya hivyo kwa kuwa kamati hiyo ina nguvu kubwa ya kikanuni ikiwamo kukamatwa.
Kubenea alisema hana wasiwasi na aliyoyasema ila anataka haki itendeke kwa kufuata kanuni na hadi sasa ana vielelezo vya kutosha kuhusu suala lake.
Dk Kashililah alieleza jana kuwa hawezi kuzungumzia kwa kina jambo hilo kwa kuwa taratibu zote za kufuata zinafahamika.
“Inawezekana ameandika, lakini mpaka ifike tuipokee. Mimi nilikuwepo Ijumaa hadi saa tano usiku sikuiona. Huenda ipo njiani ikifika tutaipokea na tutaifanyia kazi,” alisema Kashililah.
No comments:
Post a Comment