Cristiano Ronaldo amekosa mkwaju wa penati wakati wa kipindi cha pili na kuinyima ushindi timu yake ya taifa ya Ureno kwenye mchezo dhidi ya Austria na kuliacha Kundi F likiwa wazi kwa kila timu kufuzu hatua ya 16 bora.
Penati hiyo ilikuja baada ya beki Martin Hinteregger wa Austria kumwangusha Ronaldo kwenye eneo la hatari lakini mkwaju wa nyota huyo wa Real Madrid uligonga ‘nondo’ kabla ya kufunga goli ambalo lilikataliwa kwasababu tayari alikuwa yuko kwenye eneo la kuotea.
Shukrani nyingi zinaenda kwa golikipa wa Austria Robert Almer, ambaye alifanya kazi ya ziada kuokoa michomo ya hatari.
Aliokoa mpira wa kichwa wa Ronaldo pamoja na shuti la Nani ambaye alipiga kichwa kilichogonga mwamba mapema kipindi cha kwanza wakati Ureno ikipambana kupata ushindi wa kwanza kwenye michuano ya Euro 2016.
Ureno walitawala mchezo huo uliozikutanisha nchi hizo mbili kwa mara ya kwanza kwenye mechi ya mashindano tangu 1995 lakini mara kadhaa pia Ureno walinusurika kuchapwa hasa pale Stefan Ilsanker alipotandika mkwaju dakika chache baada ya kipindi cha pili kuanza.
Matokeo hayo yanaiweka Hungary kileleni mwa Kundi F kwa pointi nne, Ureno na Iceland kwa pamoja zinapointi mbili na Austria ikiwa na pointi moja hali inayofanya timu zote nne kuwa na na nafasi ya kufuzu kucheza 16 bora ya mashindano hayo.
Dondoo muhimu
- Cristiano Ronaldo amekosa penati kwa mara ya kwanza kwenye michuano mikubwa (ndani ya dakika 90) (alifunga dhidi ya Iran mwaka 2006 kwenye kombe la dunia. Amekosa nne kati ya tano akiichezea timu ya taifa na klabu.
- Ronaldo amekuwa mchezaji wa kwanza wa Ureno kukosa penati kwenye michuano mikubwa ndani ya muda wa kawaida.
- Ronaldo amekuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi kwenye kikosi cha Ureno (mechi 128) akivunja rekodi ya Luis Figo (alicheza mechi 127).
- Austria wamecheza mechi yao ya kwanza bila kuruhusu goli kwenye mashindano makubwa ndani ya mechi 14 na ni mara ya kwanza tangu mwaka 1982 dhidi ya Algeria.
- Ureno haijapoteza mchezo wowote dhidi ya Austria kwenye mechi tano zilizopita, mechi nne kati ya hizo ni sare, wameshinda mchezo mmoja.
No comments:
Post a Comment