MKOA wa Rukwa umebaini watumishi hewa 647 ambao wanadaiwa kusababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 3.6.
Idadi hiyo ni watumishi hewa waliokuwa wakilipwa mshahara kati ya Julai 2013 na Mei 2016.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Mussa Kunenge alisema hayo katika mkutano wa viongozi wa dini, ambao Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Zelothe Steven alitumia fursa hiyo kujitambulisha kwa viongozi hao wa kiroho.
Katika mkutano huo, Katibu wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste mkoani humo, Mchungaji Henry Chomola alitaka kujua idadi ya watumishi hewa waliobainika mkoani humo.
“Watumishi hewa ni tatizo, wanaingizia serikali hasara kubwa, mie ni shahidi , nimestaafu lakini bado napandishwa cheo, hii haifai kabisa “ alisisitiza na kumtaka Kaimu Katibu Tawala kutoa taarifa.
Kwa mujibu wa Kunenge, Sh bilioni 3.6 zilizolipwa kwa watumishi hao hewa, zingeweza kutengeneza zaidi ya madawati 73,000 kwa shule za msingi na sekondari.
Alisema kuwa watumishi hewa wapatao 492, ambao walisababisha hasara ya Sh 2, 276 , 643 , 620 waliondolewa kwenye mfumo wa malipo kabla ya Machi 2016 .
“Watumishi hewa 155 ambao wameingiza hasara ya Sh 1,392,760, 660 wameondolewa kwenye mfumo wa malipo baada ya agizo la Rais John Magufuli la mwezi Machi mwaka huu lililowataka wakuu wa mikoa nchini kuhakiki watumishi hewa mikoani mwao, “ alieleza.
No comments:
Post a Comment