Maliasili, Utalii sasa kuendeshwa ‘kijeshi’ - PATRICIA-TV.com

Breaking

Share daily activities and have all funs here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Thursday, June 23, 2016

Maliasili, Utalii sasa kuendeshwa ‘kijeshi’

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, ametangaza kuwapo mageuzi katika mamlaka za hifadhi za Taifa, mamlaka za maliasili na mamlaka ya wanyamapori kutoka mfumo wa uendeshaji wa kiraia na kuwa wa Jeshi Usu.

Mfumo huo mpya wa Jeshi Usu unalenga kuweka umadhubuti wa kukabiliana na vitendo vya ujangili, usafirishaji wanyamapori hai, uingizaji wa mifugo katika hifadhi na shughuli nyingine zikiwemo za uchomaji mkaa, ukataji magogo, uchimbaji madini na vingine vinavyotishia kutoweka rasilimali za taifa.

Alisema hayo wakati akifungua mkutano wa siku mbili kwa Watendaji Wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake, uliofanyika juzi mjini hapa.

Waziri alisema, tayari mpango huo umeanza kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) baada ya watendaji wake wakuu na wahifadhi wakuu na askari wa shirika hilo kupatiwa mafunzo ya kijeshi Usu kuhusu namna ya kulinda hifadhi za taifa kutokana na kuwepo kwa uvamizi wa mifugo na idadi kubwa ya majangili.

Alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2016/2017, Wakala wa Misitu Tanzania(TFS) utageuzwa kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Misitu kuundiwa bodi yake.

Mbali na hayo alisema, baada ya kuwa mamlaka, watendaji wake watapatiwa mafunzo ya kijeshi na kuwa Jeshi Usu litakalokuwa na jukumu la kulinda hifadhi za misitu za taifa.

Pia amekemea vitendo vya baadhi ya watendaji wa wizara hiyo na idara zake kushirikiana na wahalifu kuhujumu maliasili za taifa kwa manufaa yao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii, Atashasta Nditiye, alisema sekta hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uvamizi wa mifugo kwenye hifadhi, ujenzi wa makazi na migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

Awali, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali mstaafu, Gaudence Milanzi, alisema wizara imepokea hoja na changamoto kutoka kwa wabunge katika bajeti ya wizara hiyo na imejipanga kuhakikisha zinatekelezwa kulingana na maagizo yatakayotolewa na Waziri.

Milanzi alisema licha ya Sekta ya Maliasili na Utalii kukabiliana na changamoto zilizopo, wizara itaendelea kuboresha sekta hiyo kupitia malengo na mipango iliyopo ili kusaidia kukuza uchumi wa Taifa zinazotokana na rasilimali zilizopo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here