SERIKALI imesema muda si mrefu inatarajia kuanza kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha za ndani kwa asilimia 100, kutokana na washirika wa maendeleo kuanza kupunguza ufadhili na misaada katika miradi hiyo.
Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ludewa, Deo Ngalawa(CCM), aliyetaka kujua ni lini serikali itaacha kutegemea wafadhili katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Ngalawa pia alitaka kujua ni lini serikali itajenga miundombinu ya umwagiliaji nchi nzima ili kuboresha kilimo cha umwagiliaji. Lwenge alisema kwa sasa washirika wa maendeleo wamepunguza kusaidia miradi ya maendeleo, jambo ambalo limeifanya serikali kujipanga kuanza kutekeleza miradi ya maendeleo kwa fedha za ndani kwa asilimia 100.
Akijibu swali la pili la nyongeza la Ngalawa, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe alisema zipo hekta milioni 29.4 za kutekeleza miradi ya umwagiliaji kwa kuziwekea miundombinu na kwa mwaka huu, hekta milioni 12 zitajengwa miundombinu ya umwagiliaji.
Katika swali la msingi, Ngalawa alitaka kujua mpango wa serikali wa kuliendeleza bonde la Mto Ruhuhu lililopo katika kata ya Ruhuhu wilaya ya Ludewa, ambalo ni eneo muhimu sana na linaweza kuzalisha mazao mengi na kupunguza uhaba wa chakula Tanzania.
Kamwelwe alisema Serikali inatambua umuhimu wa bonde hilo, ambapo katika maandalizi ya uendelezaji wa bonde hilo upembuzi wa awali ulifanyika kati ya mwaka 2013 na 2014.
Alisema walibaini uwezekano wa kujenga bwawa kubwa katika eneo la Kikonge kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo kudhibiti mafuriko katika bonde la mto Ruhuhu, kuendesha kilimo cha umwagiliaji kwa eneo la takribani hekta 4,000 na kufua umeme mkubwa utakaounganishwa kwenye gridi ya Taifa.
Alisema kwa sasa serikali kwa kushirikiana na benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ipo katika hatua ya kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa bwawa na miundombinu ya umwagiliaji.
No comments:
Post a Comment