HATIMAYE TAKUKURU NA TRA WAMTAJA MTU ALIYEKUWA AKIIBIA SERIKALI MILIONI 7 KWA KILA DAKIKA. - PATRICIA-TV.com

Breaking

Share daily activities and have all funs here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Thursday, June 30, 2016

HATIMAYE TAKUKURU NA TRA WAMTAJA MTU ALIYEKUWA AKIIBIA SERIKALI MILIONI 7 KWA KILA DAKIKA.


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) hatimaye wametaja mfanyabiashara ambaye alibainishwa na Rais John Magufuli katika hafla ya kuwaapisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Ikulu Dar es Salaam juzi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentino Mlowola alimtaja mfanyabiashara huyo kuwa ni Mohammed Mustafa Yusuf Ali anayetuhumiwa kuiibia Serikali matrilioni ya shilingi kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs) ambazo hazijasajiliwa na TRA na kutoa risiti bandia.

Alisema TRA kwa kushirikiana na TAKUKURU inaendelea na uchunguzi ili kubaini makampuni yote yanayojihusisha na udanganyifu huu, ambapo hadi sasa jumla ya makampuni manne yamebainika kujihusisha na ukwepaji kodi kwa mtindo huu kuanzia mwaka 2010 hadi 2014; na jumla ya Sh 29,216,900,301.7 imebainika kutokulipwa serikalini na makampuni hayo kwa kipindi hicho.

Alisema kwa sasa wanaendelea na mahojiano naye zaidi ili kuwabaini wote wanaohusika na mfumo huo na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa TRA, Alfayo Kidata aliyeambatana na Mlowola katika mkutano huo wa waandishi wa habari, makampuni hayo yamekuwa yakinunua risiti za manunuzi bandia kutoka kwa watu wanaomiliki mashine za EFDs ambazo hazijasajiliwa.

“Makampuni hayo wakishanunua risiti za manunuzi bandia, hatimaye huzitumia risiti hizo kudai marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) bila kuwepo na bidhaa au huduma halisi iliyouzwa au kutolewa na mhusika, kitendo ambacho kinainyima serikali mapato stahiki kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Aliyataja makampuni hayo kuwa ni pamoja na Skol Building Material Ltd ambayo tangu mwaka 2012 hadi 2013 haikulipa jumla ya VAT ya Sh 5,464,915,963 na Kodi ya Mapato yenye thamani ya Sh 10,960,787,861 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh 16,425,703,824 kwa kipindi hicho.

Kampuni nyingine ni Farm Plant (T) Limited ambayo tangu mwaka 2010 hadi 2014 haikulipa jumla ya VAT ya Sh 5,930,170,573 na kodi ya mapato yenye thamani ya Sh 4,948,393,516 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh 10,878,564,089.

Pia imo kampuni ya A.M.Steel & Iron Mills Limited ambayo kuanzia mwaka 2013 hadi 2014 haikulipa jumla ya VAT ya Sh 79,016,112 na kodi ya mapato yenye thamani ya Sh 131,693,518 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh 210,709,630.

Kampuni nyingine ni A.M Trailer Manufacturers Limited ambayo tangu mwaka 2013 hadi 2014 haikulipa VAT ya Sh 638,221,034.80 na kodi ya mapato yenye thamani ya Sh 1,063,701,724. 00 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh 1,701,922,758.00.

Alisema baada ya kubaini ukwepaji kodi huo kwa kushirikiana na TAKUKURU inaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizo na mara baada ya uchunguzi kukamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukwepa kodi.

Alitoa mwito kwa wafanyabiashara wote kutojihusisha na kununua risiti za bandia na kudai marejesho ya VAT yasiyostahili kwa kuwa mamlaka imejizatiti kuendelea kuwabaini wafanyabiashara wanaokwepa kodi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa hatua stahiki.

Aidha alisema uchunguzi wa awali pia umebaini kuwepo makampuni hewa 228 na kusisitiza kwamba wameusimamisha mfumo huo bandia na kutoa siku tatu kwa kampuni zote zinazodaiwa kulipa fedha hizo.

“Hakuna yeyote anayekwepa kodi atasalimika, wote ni lazima walipe na sasa tumedhibiti mfumo huo bandia,” alisema.

Juzi Magufuli akizungumza na Ma RC na Ma DC wapya, aliwataka wakasimamie vyema mapato katika maeneo yao kwani kumekuwepo na baadhi ya watu wajanja wanaotumia vibaya taasisi za Serikali ikiwemo Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brela) TRA kujinufaisha wenyewe na kuliingizia taifa hasara.

Alisema: “Tulikuwa tunafuatilia mashine za EFDs zinazokusanya mapato, yupo mtu mmoja alitengeneza kampuni nyingi zilizokuwa zikimlipa asilimia tano ya VAT na yeye anacheza na TRA halipi asilimia 18 ya kodi hiyo. Alikuwa anaingiza kati ya shilingi milioni saba mpaka nane kwa dakika. Serikali ilipoteza matrilioni ya fedha. Huyu mtu yupo kwenye mikono salama kwa sasa”.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here