Shule Binafsi Marufuku Kutoza Ada ya Majengo – Ndalichako Serikali imezitaka shule binafsi kuacha kuwatoza wazazi fedha kwaajili ya majengo kwani kazi hiyo ni ya mmiliki wa shule na anatakiwa awe amekamilisha ujenzi kabla hajafungua shule yake.
Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Joyce Ndalichako jijini Dar es Salam wakati akizungumza na waandishi wa habari. Dkt. Ndalichako aliongeza na kusema kuwa kuwatoza fedha hizo wazazi ni kuwabebesha mzigo ambao hauwahusu kwani wanachotakiwa kufanya ni kulipa ada kwa ajili ya watoto wao. Waziri huyo amesema serikali kupitia kwa Kamishna wa Elimu nchini itapitia michanganuo yote ya ada na michango mbalimbali inayotozwa na shule binafsi nia ikiwa ni kuiondoa michango isiyokuwa ya lazima ili kuwapunguzia wazazi mizigo ambayo wanabebeshwa; mingine isiyowahusu.
Amesema ili kukabiliana na Changamoto hiyo amewataka wamiliki wa shule hizo kuwasilisha michanganuo ya ada na michango mingine ili iangaliwe kipi kinaulazima wa kuendelea kulipiwa na mzazi na kitu gani kuondolewa; au kibebwe na wamiliki wa shule hizo. “Utakuta shule inamtaka mzazi kulipia shilingi 90000 kwa ajili ya majengo, hayo majengo mtoto wake akimaliza yanamsaidia nini?” alihoji waziri Ndalichako. Akieleze kuhusu suala la ada elekezi alisema kuwa jambo hilo lilifanywa na bunge la kumi lakini kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza ilionekana hakuna haja ya kuliendeleza.
Amesema kwa sasa serikali inampango wa kuzipitia shule hizo na kuzipanga kwa madaraja ambayo hata hivyo hakuelezea madaraja hayo yatakuwa na lengo gani. Wakati huo huo, Waziri Ndalichako amesema hoja ya lugha ipi iwe yakufundishia mashuleni kati ya Kiswahili na Kiingereza litapelekwa kwa wadau ambao ndiyo watatoa uamuzi. Amesema pamoja na kuwa Kiswahili ndiyo kinaonekana kuwa lugha rahisi kwa walio wengi, maandalizi mazuri pia ndiyo suluhisho kwa lugha ya Kiingereza.
No comments:
Post a Comment