Hatua ya makundi ya Euro 2016 sasa imekwisha na timu 16 pekee zimebaki kwenye mashindano. Timu ya Wales ilishangaza wengi pale ilipoongoza kundi lake hasa ukizingatia kwamba hii ilikuwa michuano yao ya kwanza ya Euro. Croatia nao walizidi kupata nguvu kadri michuano ilivyoendelea walicheza mechi nzuri zaidi kwenye michuano hii walipompiga bingwa mtetezi Spain 2-1
Wenyeji France, mabingwa wa Dunia Ujerumani na Italy nao waliongoza makundi yao na kufuzu kwenda hatua nyingine, pia Hungary waliweza kufanya hivyohivyo.
Tutazame timu bora ya hatua ya makundi Euro 2016.
GOLIKIPA
Michael McGovern
Wengi hawakumtambua mchezaji huyu kuelekea kwenye hii michuano ila aliweza kuona nyota yake iking’aa kutokana na uwezo wake aliouonesha kwenye mechi dhidi ya timu ya Ujerumani. Alidaka mara 15 kwenye mechi hii na pia alisaidia timu yake kwenye mechi nyingine kwenye hatua hii ya makundi.
MABEKI
Darjo Srna
Kaptain huyu wa Croatia ambaye alifiwa na baba yake katikati ya mashindano haya alicheza vizuri sana kwenye mechi zote za timu yake. Srna alirudi nyumbani kwa ajili ya msiba wa baba ake ila aliweza kucheza mechi zote tatu.
Jerome Boateng
Kimya kimya Boateng ameweza kujiwezesha kuwa beki bora zaidi duniani na ameweza kuonesha ubora wake kwa mara nyingine tena kwenye michuano hii ya Euro. Boateng alisaidia timu yake kupata clean sheet mbili huku akikamilisha asilimia 87 ya pasi zake.
Leonardo Bonucci
Beki huyu mstaarabu na mzoefu ameweza kung’aa sana kwenye timu ya Azzuri. Wengi bado wanakumbuka pasi yake kwa Emanuel Giaccherini iliyozalisha goli la kwanza kwenye mechi ya Italy dhidi ya Belgium.
Kyle Walker
Alikuwa kati ya wachezaji wachache wa England walioweza kufanya vizuri sana mpaka sasa. Mashambulizi mengi ya England yalipitia kwake na hakika England walibidi waweke golini krosi yake angalau hata moja ambazo alikuwa akiweka ndani ya boksi kwenye mechi zote tatu.
VIUNGO
Eric Dier
Beki huyu aliyegeuzwa kuwa kiungo kwenye timu ya England ndiye mchezaji bora wa timu ya England mpaka sasa hivi. Amelinda mabeki wake vizuri na hata anatoa mchango kwa timu yake inapoenda mbele. Dier alifunga ‘free-kick’ kwenye mechi ya kwanza ya England dhidi ya Russia
Toni Kroos
Kama ilivyokuwa kawaida yake Kroos hakufanya kosa lolote kwenye safu ya kiungo ya Ujerumani. Huyu ni mmoja kati ya viungo bora zaidi duniani na inaonekana ukimtazama akipiga pasi zake hapa na pale na kufanya timu ya Ujerumani icheze vizuri. Hakika alistahili kuwa mchezaji bora kwenye ushindi wa 2-0 wa Ujerumani dhidi ya Ukraine.
Iniesta
Akicheza michuano yake ya kwanza bila msaidizi wake Xavi, wengi walidhani kwamba Iniesta hatoweza kufanya vizuri kama ilivyokuwa huko nyuma hasa ukizingatia kwamba umri wake umeenda. Iniesta ameweza kuwanyamazisha wote kwa kuonesha kiwango cha hali ya juu kwenye michuano hii. Ametengeneza nafasi lukuki za magoli na hakika wakiwa na Iniesta kwenye timu yao, Spain wanaweza kufika mbali kwenye mashindano haya.
WASHAMBULIAJI
Dimitri Payet
Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps hakupenda kumtumia mchezaji huyu, ila uwezo aliounesha kwenye timu ya West Ham msimu huu ulimzawadia bahati Payet kuitwa kwenye timu ya Taifa na hakika Payet hakuangalia nyuma tena. Huyu ndiye mchezaji bora wa michuano hii mpaka sasa akiwa na magoli mawili.
Gareth Bale
Mchezaji huyu wa Madrid alikuwa akiongea sana kuelekea kwenye michuano na hakika ameweza kuyatetea maneno yake uwanjani. Bale alifunga kwenye mechi zote tatu za timu yake huku magoli yake mawili yakiwa ‘Free-kick’ na kuisaidia Wales kushinda Group B.
Alvaro Morata
Mshambuliaji huyu anayesakwa na klabu nyingi, ameweza kuongeza sifuri kadhaa kwenye bei yake kutokana na uwezo aliounesha kwenye michuano hii mpaka sasa. Baada ya kucheza vibaya kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Czech Republic aliweza kurudi kwa kufunga magoli matatu kwenye mechi mbili kitu kilichochangia katika uamuzi wa klabu ya Real Madrid kuamua kumnunua tena kutoka klabu ya Juventus katikati ya Michuano.
Benchi; Perisic, Nani, Witsel, Koscielny, Modric, Xhaka, Dzsudzsak, Ramsey, Krychowiak, Hoolahan.
No comments:
Post a Comment