CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepanga kulisaidia Jeshi la Polisi kuzuia Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hivi karibuni Jeshi la Polisi lilitoa zuio la mikutano ya siasa ya wazi na ya ndani nchini kote, hata hivyo CCM imepanga kufanya Mkutano Mkuu tarehe 23 Julai mwaka huu mjini Dodoma.
Kwenye mkutano huo, Dk. Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM atakabidhi mamlaka hayo kwa Dk. John Magufuli ikiwa ni utaratibu wa kawaida wa chama hicho.
Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) limepanga kuzuia mkutano huo kwa madai ya kulisaidia Jeshi la Polisi kusimamia agizo lake kwa vyama vya siasa nchini.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Slaam viongozi wa Bavicha walisema, hatua hiyo ni katika kuhakikisha wanalisaidia jeshi kutekeleza amri iliyotolewa na Rais Magufuli ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa hadi mwaka 2020.
“Tumeandaa vijana takribani 2000 kutoka mikoa yote nchini watakaokwenda Dodoma kusaidiana na Jeshi la Polisi kutawanya mkutano usio halali wa CCM. Kwa sababau Jeshi la Polisi limezuia mikutano yote ya siasa kwa sasa.
“Pia ni katika kuunga mkono kauli ya Rais Magufuli kwamba, hakuna mikutano ya vyama vya siasa mpaka mwaka 2020. Huu ndio msiamamo wa baraza.
“Mikutano yetu sisi kama Chadema tunazuiwa lakini CCM wanafanya. Mahafari ya chama cha mapinduzi yanafanyika. Ni jana CHASO (Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Chadema) Morogoro tumezuiwa lakini UVCCM (Umoja wa Vijana wa CCM) Mkoa wa Morogogo wamefanya na picha zipo. Hii sio haki, kama mbwai na iwe mbwai,” alisema Patrick ole Sosopi, Makamu Mwenyekiti wa baraza hilo.
George Tito, Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya alisema “… ni kwamba, huko mikoani vijana wameshajipanga. Wana ari kubwa ya kwenda Dodoma.
“Tumeamua kufikia hatua hii kwa sababu tumekuwa tunaona hakuna haki katika nchi hii. Kuna mahafali yanafanyika vyuo vikuu, wenzetu CCM wanaruhusiwa sisi Chadema tunakatazwa.Vijana wa Chadema wamekuwa wakikamatwa bila sababu za msingi,” alisema Tito.
No comments:
Post a Comment