Mgombea urais wa chama cha Democratic nchini Marekani Hillary Clinton amesema ujumbe ulioandikwa na mpinzani wake Donald Trump kwenye Twitter ulieneza chuki dhidi ya Wayahudi.
Ujumbe huo wa mgombea huyo wa chama cha Republican ulikuwa na umbo linalokaribiana na nyota ya Daudi pamoja na rundo la pesa.
Ndani ya umbo hilo, kulikuwa na maandishi yaliyoeleza kuwa Bi Clinton ndiye “mgombea mfisadi zaidi kuwahi kuwepo!”
Ujumbe huo ulifuywa baadaye na badala yake akaandika ujumbe mwingine maandishi hayo yakiwa ndani ya umbo la duara.
Bw Trump alisema vyombo vya habari vina unafiki kwa kulinganisha umbo lake na umbo la Nyota ya Daudi, ishara ya Uyahudi.
"Hatua ya Donald Trump kutumia picha za chuki dhidi ya Wayahudi kutoka kwenye tovuti za kibaguzi kuendelea kampeni yake inashtua,” maafisa wa kampeni wa Bi Clinton walisema. “Lakini hali kwamba haya ni mazoea inafaa kuwatia hofu wapiga kura.”
Bw Trump alijibu kupitia taarifa kwamba hiyo ilikuwa nyota ya kawaida, ambayo pia hutumiwa sana na maafisa wa polisi.
Alisema madai kwamba ujumbe wake ulikuwa wa kibaguzi dhidi ya Wayahudi ni ya kushangaza.
Maafisa wake wa kampeni pia walikanusha habari kwamba umbo hilo alikuwa amelitoa kutoka kwa mitandao inayoeneza chuki dhidi ya Wayahudi.
Nyota ya Daudi imo kwenye bendera ya Israel na ilitumiwa na Wanazi kuwatambua Wayahudi.
No comments:
Post a Comment