Mara nyingi kunakuwa na stori lukuki zinazovuja pale inapotokea timu fulani imetolewa mashindanoni. Suala hili sasa linafukuta kwenye timu ya taifa ya Hispania, kutokana na yake yaliyokuwa yakitokea wakati wa kambi yao kwenye michuano ya Euro mwaka huu nchini Ufaransa kabla ya kutupwa nje.
Hispania ilitupwa nje ya michuano hii baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Italy kwenye hatua ya 16 bora. Taarifa za chini-chini kutoka ndani ya timu hiyo zinadai kwamba hali hiyo inaweza kupelekea wachezaji wengi kustaafu huku wengi wao wakiwa ni wale walioshiriki katika kikosi cha ubingwa cha miaka ya 2008, 2010 na 2012.
Iker Casillas anaweza kuwa mmoja wa wachezaji hao.
Kama anavyofahamika kwa jina maarufu la ‘San Iker’, Casillas alikuwa katika kikosi kilichotwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2010. Miaka ya hivi karibuni kiwango chake kimekuwa kikishuka kwa kasi sana, kiasi cha kufikia hatua ya kupoteza nafasi yake ya mlinda lango namba moja wa Hispania kwenye michuano ya Euro mwaka huu kwa David De Gea.
Del Bosque na Casillas wamemaliza vibaya
Baada ya kuambiwa kwamba hatakuwa kipa namba moja tena wa timu ya taifa ya Hispania, Iker hakifurahishwa na jambo hilo na ndipo maelewana mabaya na kocha wake yalipoanza.
Kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Cadena Ser, kocha wa Hispania Vicente Del Bosque ametanabaisha kwamba, Casillas ndiye mchezaji pekee ambaye hakumtumia ujumbe wa shukrani, kufuatia kujiandaa kuachana na nafasi yake ya ukocha mkuu wa taifa hilo wakati mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa mwezi huu.
‘Tabia yake kwa wachezaji wenzake ilikuwa sawa tu, lakini kwa safu ya bechi la ufundi haikuwa ya kuridhisha. Hasira zake za kupoteza nafasi ya kuwa kipa namba moja aliihamishia kwetu. Na ndiyo maana amekuwa ndiye mchezaji pekee ambaye sijamtumia ujumbe wa shukrani.’
No comments:
Post a Comment