RAIS wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame akiwa tayari kukabidhi tuzo kwa Wizara, taasisi za Serikali, kampuni, nchi washiriki pamoja na mashirika yaliyoshinda katika maonesho ya 40 ya biashara ya kimataifa katika uwanja wa maonesho wa Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam Ijumaa Julai 1, 2016. Kushoto kwake ni mwenyeji wake Rais Dkt John Pombe Magufuli na kulia kwake ni Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhe. CharlesMwijage akifuatiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bw. Edwin Rutageruka.
Rais Paul Kagame alikabidhi tuzo hizo Ijumaa Julai 1, 2016 wakati alipokuwa akifungua maonesho ya 40 ya biashara ya kimataifa katika viwanja vya Mwl Nyerere maarufu kama Sabasaba, vilivyopo katika barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam.
Wizara na taasisi za Serikali, kampuni pamoja na mashirika mbalimbali yalishiriki maonesho hayo kwa kushindana katika kuonesha bidhaa bora na kueleza huduma nzuri wanazotoa, ambapo baadae Rais Paul Kagame aliwakabidhi washindi hao tuzo mbalimbali.
Baadhi ya washindi hao walioganywa katika makundi mbalimbali ni pamoja na, kundi la bidhaa za kilimo nafasi ya mshindi wa tatu ilishikwa na kampuni ya farm equip Tanzania limited, nafasi ya mshindi wa pili ilishikwa na kampuni Asas dairies na nafasi ya mshindi wa kwanza ilishikwa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT).
Katika kundi la usindikaji wa vyakula na huduma za vinywaji, nafasi ya mshindi wa tatu ilishikwa na kampuni ya Bakhresa Group, ikifuatiwa na kampuni ya P&P, na nafasi ya mshindi wa kwanza ilishikwa na kampuni ya Afri tea and coffe blenders limited.
Kwa upande wa taasisi za kifedha, nafasi ya mshindi wa tatu ilishikwa na benki ya TIB, ikifuatiwa na Benki ya CRDB huku Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ikishika nafasi ya kuwa mshindi wa kwanza. Vilevile katika kundi la Mifuko ya hifadhi ya jamii nafasi ya mshindi wa tatu ilishikwa na mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF, nafasi ya mshindi wa pili ilishikwa na Mfuko wa Pensheni wa LAPF na nafasi ya mshindi wa kwanza ikiwa ni Mfuko wa Pensheni wa PPF.
Kwa upande wa nchi za kigeni zilizoshiriki maonesho hayo ya 40 tuzo zilienda kwa nchi za Rwanda iliyoshika nafasi ya mshindi wa tatu, Ujerumani ikishika nafasi ya mshindi wa pili huku nafasi ya mshindi wa kwanza ikiwa ni nchi ya Afrika Kusini. Aidha, washindi wa jumla walioshiriki katika maonesho ya 40 ya biashara ya kimataifa ya Sabasaba ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kilichoshika nafasi ya mshindi wa tatu , ikifuatia Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja Chuo cha Cha Ufundi Stadi (VETA) kilichoshika nafasi ya mshindi wa kwanza.
Baada ya kuwakabidhi tuzo hizo na kufungua rasmi maonesho hayo ya 40 ya biashara ya kimataifa Rais Kagame alitoa wito kwa washiriki wa maonesho hayo ya 40, kushirikiana ili kubuni mawazo mapya ya biashara ikiwa ni pamoja na kutambua fursa zilizopo katika soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, katika kukuza biashara zao na kusaidia ukuzaji wa uchumi wa pamoja katika nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.
No comments:
Post a Comment