Na Baraka Mbolembole
MSHAMBULIZI wa Taifa Stars, Elius Maguli amekamilisha usajili wake kutoka Stand United ya Shinyanga kama mchezaji huru na kujiunga katika klabu ya Dhofar SC ya Oman Professional League.
Kila mmoja anakumbuka namna mchezaji huyo alivyopitia kipindi kigumu msimu wa 2014/15 akiwa na kikosi cha Simba SC ambacho kabla ya kuanza kwa msimu wa 2015/16 kocha aliyepita wa kikosi hicho, Dylan Kerr alitangaza kutomuhitaji na uongozi ukavunja mkataba wake akiwa bado na mwaka mmoja zaidi.
Kitendo cha kujiunga na kocha Mfaransa, Patrick Liewig katika timu ya Stand kabla ya kuanza kwa msimu uliopita hakikuonekana kuwastua wengi lakini game 9 za mwanzo wa msimu ziliambatana na magoli 9 kwa mchezaji huyo wa zamani wa Ruvu Shooting, pia alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi katika VPL na kujumuhishwa katika timu ya Taifa kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu.
Kujiunga na Dhofar timu iliyomaliza katika nafasi ya tano katika ligi ya kulipwa mwaka mmoja uliopita ni hatua kubwa kwa mchezaji kijana kama Maguli ambaye ameondoka VPL akiwa amefunga jumla ya magoli 33 katika misimu yake mitatu aliyocheza kama mchezaji wa vilabu vya Shooting, Simba na Stand United.
Ameruka vikwazo vingi katika ‘soka lenye fitna’ na matatizo mengi ya watendaji. Mfano, katika misimu yake miwili ya mwisho VPL (Simba na Stand) timu hizo zote mbili zimejaa migogoro ya kiutendaji kati ya viongozi na wachezaji au viongozi kwa viongozi.
Katika mazingira hayo si rahisi kwa mchezaji kutimiza malengo yake na inapotokea nafasi kama hii ya Maguli-Kusajiliwa moja kwa moja na timu ya kulipwa ukiwa U25 ni jambo la kumshukuru Mungu na pengine ni sehemu ya kufanya kazi nzuri zaidi kwa jitihada ili kuthibitisha kwa wale waliokusaini kuwa hawakufanya makosa.
Maguli ni mshambuliaji wa kikosi cha kwanza katika timu ya Taifa ya Tanzania kwa mwaka mmoja sasa akicheza sambamba na Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta katika safu ya mashambulizi kwa maana hiyo, kocha Charles Mkwassa ataendelea kufurahia vijana wake watatu wakiwa ng’ambo ya nchi kuendeleza vipaji vyao na kudumisha viwango vyao vya kiuchezaji.
Kama Hamis Mroki anayecheza Thailand, huyu ni nahodha wa kikosi cha vijana kilichokuwa kikiwajumuhisha kina Ulimwengu, Himid Mao na wengine ni zao la TSA, Samatta, Tom, Maguli, Mrisho Ngassa watatupiwa jicho la 3 bila shaka timu ya Taifa Stars itaimarika licha ya kwamba bado hatuna ligi makini ya ndani.
Dhofar ni timu iliyoanzishwa miaka 44 iliyopita, na Oman kuna mishahara mikubwa hadi kufikia dola 30,000 kwa mchezaji wa kiwango cha Maguli. Mchezaji wa kikosi cha kwanza wa timu ya Taifa. Sasa mastaa watatu wa Stars katika kikosi cha mashambulizi wapo ng’ambo. Kila la heri Elius Maguli.
Kwa ukaribu zaidi, tafadhali unaweza ku-LIKE PAGE yangu BSports. Utapata Updates za michuano mbalimbali.
No comments:
Post a Comment