WAZIRI Mkuu mstaafu, John Malecela ametoa madawati 125 ambayo yatapelekwa katika wilaya ya Chamwino, ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za kuhakikisha watoto wote wa shule za msingi na sekondari wanakaa kwenye madawati.
Alikabidhi madawati hayo juzi kwa Mkuu ya Wilaya hiyo, Vumilia Nyamonga.
Malecela alisema alipata wazo la kuwa mmoja wa wachangiaji wa madawati, lakini alipopapasa mfukoni alikuwa hana fedha ndipo alipoalika marafiki zake kwenye chakula cha pamoja na kuwapa wazo hilo.
“Tukala chakula pamoja, wakati tunakunywa mvinyo nikachomekea na waliweza kuchangia madawati 125,” alisema na kuongeza kuwa juhudi za Rais Magufuli katika suala la madawati litaondoa kabisa changamoto hiyo.
Alisema madawati hayo yatapelekwa katika shule za msingi za Chamwino kwani huko ndio nyumbani kwao.
“Ugogoni kuna methali ‘mkia wa mbuzi hufagia kwanza alipolala’ nikaona madawati hayo nipeleke Chamwino,” alisema.
Katika kuunga juhudi hizo pia wakati wa hafla ya kukabidhi madawati, kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma aliunga mkono juhudi hizo na kuchangia fedha taslimu shilingi 130,000 ambazo zitatosha kununua madawati mawili.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga alisema madawati hayo yatasaidia wanafunzi 375 wa wilaya ya Chamwino waliokuwa wakikaa chini na mchango huo ni muhimu kwani utasaidia katika kuinua sekta ya elimu wilayani humo.
Alisema wilaya hiyo imefikisha asilimia 80 ya uhitaji wa madawati na bado inaendelea na jitihada za ukamilishaji wa asilimia iliyobaki ili watoto wote wakae kwenye madawati.
Nyamonga alisema Malecela mbali na kutambulika kitaifa na kimataifa kwa michango yake ya hali na mali katika shughuli za kimaendeleo, amekuwa mlezi wa wilaya hiyo na mara nyingi amekuwa chachu ya maendeleo.
Alisema waziri mkuu huyo mstaafu amekuwa akisaidia katika elimu, afya, maji, kilimo na barabara akiwa kama kiongozi na hata baada ya kustaafu na ameendelea kufanya hivyo makubwa mengi ya kimaendeleo ndani ya wilaya.
No comments:
Post a Comment