WALIOFICHUA UOVU WAAHIDIWA ULINZI - PATRICIA-TV.com

Breaking

Share daily activities and have all funs here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Monday, May 29, 2017

WALIOFICHUA UOVU WAAHIDIWA ULINZI

MKUU wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amewataka wachimbaji wadogo waliofichua maovu ya watendaji wa Ofisi ya Madini kwa kushirikiana na Kampuni zilizopewa leseni za kuchimba madini katika eneo la Kitunda wilayani Sikonge, kamwe wasiwe na wasiwasi kwani Serikali itawashika mkono ili wasidhurike.
Alitoa kauli hiyo jana katika eneo la Kitunda kwenye mkutano wa hadhara uliohusisha wachimbaji hao, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya ya Sikonge na viongozi wa kampuni zenye leseni ya uchimbaji wa madini.

Alisema hayo baada ya malalamiko kuwa wachimbaji hao waliosema wamekuwa wakipata vitisho kutoka kwa wamiliki wa migodi na baadhi ya watendaji. Alisema wamefanya vyema kusema ukweli na kufichua maovu yanayoendelea katika eneo la machimbo hayo.

Alisisitiza Serikali inawahakikishia ulinzi na kwamba hakuna yeyote atayenyanyaswa katika eneo hilo. Alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Sikonge kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Sikonge, kuhakikisha vijana wote walioeleza uovu wa watendaji wa Ofisi ya Madini ya Mkoa kwa kushirikiana na kampuni za madini wanakuwa salama na kuendelea na kazi zao.

Alionya waliohusishwa na uovu, kamwe wasijaribu kuwagusa vijana walioeleza matatizo mbalimbali yanayowakabili. Mmoja wa wachimbaji hao, Linus Saidi alidai kampuni moja (jina tunalo) imekuwa ikiwanyanyasa wachimbaji madini, wanaonekana kutetea haki za wenzao na kufichua maovu yanayoendelea katika eneo hilo kwa kuwafukuza na kuyafukia mashimo yao.

Alisema uovu mwingine unafanywa na kampuni hiyo, kufukua mashimo (maduara) yaliyozuiwa na Serikali kwa hofu za usalama wa wachimbaji wadogo na kuendelea uzalishaji, lakini wanapotokea viongozi huyafunika kwa kuweka majani na miti ili mahali husika paonekane hapatumiki.

Mchimbaji mwingine, Simon Chacha alisema baadhi ya watendaji kutoka Ofisi ya Madini Mkoa wa Tabora, wamekuwa wakishirikiana na kampuni hiyo katika kuwakandamiza wananchi na kutorosha mapato ya serikali kwa kutoa taarifa zisizo halisi za kiwango cha dhahabu iliyozalishwa.

Aliongeza kuwa mmoja wa watendaji wa Ofisi ya Madini, ameongezwa kuwa mwanahisa wa kampuni inayotuhumiwa, hatua inayosababisha kuficha takwimu za uzalishaji. Mkuu wa Mkoa aliahidi kufuatilia tuhuma hizo na alisema ikibainika ni kweli, kila mmoja atachukuliwa hatua kulingana na alivyohusika kwenye tuhuma zilizotajwa.

Aliwaomba vijana hao kutoa ushirikiano kwa Serikali wakati itakapokuwa ikiendelea kufuatilia tuhuma mbalimbali zilizoelezwa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here