Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 28 Mei, 2017 aliwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya Mwaisela iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuwashukuru Madaktari na Wauguzi kwa juhudi kubwa wanazofanya kunusuru maisha ya watu.
Mhe. Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli wamewatembelea wagonjwa hao majira ya saa moja ya asubuhi wakitokea katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay Jijini Dar es Salaam ambako wamehudhuria ibada ya Jumapili.
Miongoni mwa wagonjwa waliojuliwa hali na Mhe. Rais Magufuli na mkewe ni Mzee Francis Maige Kanyasu (Ngosha) aliyelazwa katika chumba namba 310 na Mtoto Shukuru Musa Kisonga aliyelazwa katika chumba namba 312 ambaye hivi karibuni aliripotiwa kuugua ugonjwa usiofahamika uliosababisha aishi kwa kunywa mafuta ya kula, sukari na Maziwa.
Pamoja na kuwapa pole wagonjwa waliolazwa katika wodi ya Mwaisela na kuwashukuru Madaktari na Wauguzi, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali itaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili hospitali hiyo na changamoto zinazowakabili madaktari na wauguzi.
“Jamani, Madaktari tunawashukuru sana, mnafanya kazi nzuri, Madaktari wote nchini pokeeni pongezi zangu, sisi Serikali tutaendelea kuzikabili changamoto hizo na siku moja zitakwisha, kikubwa ni kumtanguliza Mungu mnapofanya kazi ya kuokoa maisha ya watu kwa juhudi kubwa, mnafanya kazi ya Mungu” alisema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru alimshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwatembelea wagonjwa katika hospitali hiyo na amemhakikishia kuwa Madaktari tayari wamegundua magonjwa yanayowakabili Mzee Francis Maige Kanyasu (Ngosha) na Mtoto Shukuru Musa Kisonga na kwamba wanaendelea vizuri na matibabu.
Aidha, Prof. Museru amesema hospitali hiyo imepiga hatua kubwa ya kujenga uwezo wa kutibu magonjwa ambayo wagonjwa walilazimika kwenda kutibiwa nje ya nchi na hivyo kuokoa fedha nyingi za Serikali.
“Mhe. Rais hospitali yetu sasa imeanza kufanya upasuaji na kutoa tiba ya magonjwa ambayo yalilazimu wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi, mfano hivi sasa tunatoa huduma ya kusafisha figo kwa wagonjwa takribani 250, na kuanzia mwezi Julai mwaka huu tutaanza kupandikiza figo.
“Huduma hii hugharimu kati ya Shilingi Milioni 60 na Shilingi Milioni 70 kwa mgonjwa mmoja anayekwenda kutibiwa nje ya nchi, lakini hapa nchini gharama zinashuka hadi Shilingi Milioni 21” amesema Prof. Museru.
Prof. Museru aliongeza kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili pia inajipanga kuanza kutoa huduma ya matibabu kwa watoto wenye matatizo ya usikivu ambao wapo hatarini kuwa viziwi na hivyo kuokoa fedha nyingi zinazotumika kuwatibu nje ya nchi, kutoka Shilingi Milioni 90 hadi Shilingi Milioni 30.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Mkewe Mama Janeth Magufuli wakimjulia hali Mzee Francis Maige Kanyasu(Ngosha) aliyelazwa Wodi ya Mwaisela katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya Matibabu. Wakwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Profesa Lawrence Museru pamoja na Dkt. Juma Mfinanga Daktari Bingwa wa magonjwa ya Dharura na Ajali katika hospitali hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mzee Francis Maige Kanyasu(Ngosha) aliyelazwa Wodi ya Mwaisela katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya Matibabu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Mkewe Mama Janeth Magufuli wakimjulia hali mtoto Shukuru Kisonga aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Mtoto Shukuru alikuwa akidaiwa kuishi kwa kula Sukari, Maziwa na mafuta ya kula lakini hali yake imeimarika zaidi na kuanza kula vyakula vya kawaida. Katikakati ni Mama yake Shukuru Mwanahabibi Mohamed Mtei.
No comments:
Post a Comment