Mechi ya kwanza ya hatua ya makundi CAF Champions League ilikuwa mbaya kwa mabingwa mara nane wa kihistoria, Al Ahly ya Misri na kwa hakika ilikuwa ni mechi nzuri na iliyotengeneza historia nzuri kwa mabingwa wa ligi kuu ya Zambia, Zesco United ambao walikuwa wakicheza kwa mara ya kwanza kihistoria hatua ya makundi ‘nane bora’ ya ligi ya mabingwa Afrika.
“Ushindi wetu umepokelewa kwa furaha kubwa na raia wa hapa (Zambia), kwanza hawakutegemea kama tungeweza kupata ushindi kutokana na idadi ya wachezaji muhimu kutokuwapo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi,” anasema straika wa timu ya Taifa ya Tanzania, Juma Ndanda Liuzio wakati nilipofanya naye mahojiano Jumatano hii akiwa nchini Zambia.
“Nimerejea uwanjani na tayari nimeitumikia timu yangu katika mechi zisizopungua tano katika ligi kuu. Game ya Al Ahly sikucheza kwa kuwa CAF haijatoa majibu baada ya jina langu kupelekwa kama nyongeza ya wachezaji wapya.”
Zesco United itacheza na Dynamo katika game ya ligi kuu leo Jumatano na hadi sasa wanashika nafasi ya tatu katika msimamo nyuma ya Zanaco wanaoshikilia usukani.
“Mechi ijayo ya CAF tutacheza ugenini dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco tarehe 28. Malengo yetu makubwa ni kufika fainali katika michuano ya mwaka huu. Uwezekano huo upo, maana tumepanga kushinda game zote 3 za nyumbani. Pointi 9 kisha hata draw moja ugenini itatosha kutupeleka nusu fainali,” anasema Liuzio ambaye hajafunga goli lolote hadi sasa.
Ushindi wa 3-2 siku ya Jumamosi iliyopita umewasaidia Wazambia hao kuongoza kundi la kwanza katika Champions league.
No comments:
Post a Comment