Watumishi wazembe kufukuzwa kazi - PATRICIA-TV.com

Breaking

Share daily activities and have all funs here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Thursday, June 23, 2016

Watumishi wazembe kufukuzwa kazi


SERIKALI imesema itawaondoa watumishi wa umma wanaokwenda kinyume na misingi, maadili ya utumishi wa umma uliotukuka wakiwemo watakaoshindwa kutatua kero za wananchi kwa wakati.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki alisema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa serikali wa ofisi ya Katibu Tawala mkoa wa Arusha, na Halmashauri ya Jiji la Arusha, katika siku ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma barani Afrika.

Alisema watumishi wanaposhirikishwa kwenye masuala yanayowagusa huboresha huduma kwa wananchi, hivyo kuongeza tija na ufanisi kazini kutokana na kufanya kazi kwa ari kubwa.

Alisema mkakati wa serikali ni kuwashirikisha watumishi kwenye majadiliano, hivyo kuleta mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Alisema hiyo inatokana na serikali kuthamini nafasi ya watumishi wa umma kama nguzo muhimu ya kufanikisha malengo ya kuwahudumia wananchi.

Alisema Wiki ya Utumishi wa Umma barani Afrika inatumika kutambua mchango wa watumishi wa umma katika kuleta maendeleo ya nchi, kupokea mrejesho kutoka kwa wadau wanaohudumiwa na serikali.

Aliwataka watumishi wa umma kutoa huduma bora iliyotukuka hivyo wahakikishe wanaongeza ari, tija katika kuwahudumia wananchi, ili wapate kuongeza matarajio na matumaini kwa serikali yao kwani wao ndio wadau wakuu wa serikali.

Kairuki alisema Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo kaulimbiu yake kwa mwaka huu ni ‘Uongozi wa umma kwa ukuaji jumuishi kuelekea katika Afrika tunayoitaka’, inatumika kutambua michango ya watumishi wa umma katika kuleta maendeleo ya nchi.

Alisema serikali imekuwa ikifanya mabadiliko ya kiutendaji katika nyanja zote kuweka mazingira bora, rafiki na wezeshi kwa watumishi wake.

Alisema lengo ni kuwafanya watumishi wake wafanye kazi kwa bidii na wawapatie wananchi huduma bora wanazozihitaji na kwa wakati. Kairuki alisema moja ya majukumu yake ni kukutana na watumishi ili awasikilize na kupata ushauri kuhusu kuboresha utendaji na tayari wizara imeanzisha dawati la msaada kwa watumishi wenye kero mbalimbali.

Aliutaka mkoa wa Arusha, halmashauri zake kuanzisha madawati ya kupokelea kero za watumishi na kuzipatia ufumbuzi, hatua ambayo ni muhimu kwa sababu wapo watumishi wanaohisi kuonewa lakini hawana pa kufikisha kilio chao.

Alisema anatambua wapo watumishi wa umma wamepewa dhamana kubwa lakini utoaji wa huduma unatiliwa shaka hawapendi kusikiliza matatizo ya watumishi.

Kadhalika Waziri Kairuki amewataka watumishi wote wa umma wajirekebishe na waishi maisha ya kazi kama mkataba wao wa huduma kwa mteja unavyosema. Amewataka wale watumishi ambao hawajajaza fomu za tamko la ahadi ya uadilifu kufanya hivyo haraka iwezekanavyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here