SIKU moja baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuweka jiwe la msingi la mradi wa ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma, kwa mara ya kwanza ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 72 imeweza kutua na kuondoka katika uwanja huo.
Jambo hilo limetafsiriwa kuwa ni mwanzo wa mashirika ya ndege kuwa na ratiba za safari za Dodoma kwani ndege zilizokuwa zikitua katika uwanja huo ni zile ndogo. Ndege hiyo ya kampuni ya ndege ya Precision Air ATR 72, ilitua juzi asubuhi ambapo miongoni mwa abiria wake alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein.
Wengine ni pamoja na Waziri wa Katiba, Sheria na Utawala Bora Zanzibar, Haruna Ally Suleiman na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe Juma.
Wakizungumza, Haruna Ally Suleiman yeye alisema amefurahi kufika Dodoma kwa kutumia ndege hiyo, hali inayoashiria juhudi za Rais John Magufuli katika kuimarisha miundombinu ya usafiri, ikiwemo usafiri wa anga. “Ni jambo la kuipongeza serikali ya Rais Magufuli tuendelee kumuombea ili maendeleo ya kweli yaweze kupatikana,” alisema.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Riziki Pembe Juma alisema ni jambo la kujivunia kuona kuna uwanja mzuri wa ndege hali inayoashiria serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Rais Magufuli inatekeleza kwa vitendo ahadi zake.
Rubani wa ndege hiyo, Kapteni Kelvin Chibole alisema kiwanja hicho kimetengenezwa vizuri na kwamba wanashukuru kwa kazi kubwa iliyofanyika na marekebisho yote yatakapokamilika kiwanja hicho kitakuwa katika hali nzuri sana.
“Kazi waliyofanya ni nzuri, marubani wengine waanzishe safari za kuja Dodoma ili kusafirisha abiria,” alisema na kuongeza kuwa anaweza kuwashawishi marubani wengine waanzishe safari za Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa wa Viwanja vya Ndege, George Sambali alisema ndege hiyo ATR 72 imetua na kuondoka kwenye uwanja huo ambapo mpaka sasa upanuzi wake ni kilometa mbili na utakapofikia kilometa mbili na nusu ndege kubwa kama za Fast Jet zenye uwezo wa kubeba abiria 150 zinaweza kuanza kuja Dodoma.
Alisema ndege kubwa zitakapoanza safari za kufika Dodoma hata bei ya usafiri itakuwa nafuu zaidi.
No comments:
Post a Comment