JESHI la Polisi kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limekana kuwa kuna watu waliovunjwa miguu waliopo kwenye chumba cha watuhumiwa kilichopo kituoni na kusema anayetakiwa kusema kuwa kuna watuhumiwa waliovunjwa miguu au mikoni ni daktari, anaandika Josephat Isango.
Simon Sirro, Kamanda wa Polisi kanda maalumu ameliambia MwanaHALISI Online kuwa katika chumba cha watuhumiwa kituoni humo hana taarifa kama kuna watu waliovunjwa miguu na kama wapo jeshi la polisi huwa linawapeleka kwenye matibabu.
MwanaHALISI online lilitaka kupata ufafanuzi ikiwa hao watuhumiwa wanapata haki ya kupata matibabu na kwanini hawafikishwi mahakamani kwa kipindi kirefu vile kinyume na sheria za nchi zinavyoelekeza wajibu wa polisi kwa watuhumiwa.
Sirro alipoulizwa kuhusu baadhi ya watuhumiwa kukaa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani, alianza kuongea na simu nyingine na kukata ya mwandishi aliyekuwa na shauku ya kutaka kujua hatima ya hao watuhumiwa.
30 June mwaka huu akizungumza waandishi wa habari baada ya kuachiwa kwa dhamana, katika mahakama ya Kisutu, Tundu Lissu Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliwataka watetezi wa haki za binadamu na mawakili kupaza sauti ili haki za hao watanzania ziweze kutambuliwa.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) aliwataja Abdalah Bushiri, na Adnani Mohamed Mrutu kutoka Same ambao wamevunjwa miguu na wanateseka katika chumba hicho bila kufikishwa mahakamani au kupelekwa kwenye matibabu.
“La Pili ni juu ya wale niliowakuta kule shimoni, na nilioshinda nao usiku wa kuamkia leo, pale Central kuna watu wamekaa wengine wiki mbili, wengine wiki tatu, na wengine mwezi, kinyume na sheria ya Tanzania inavyoelekeza kuwa mtuhumiwa afikishwe mahakamani ndani ya saa 24, isipokuwa kama ni Jumamosi na Jumapili ambazo sio siku za kazi” alisema Lissu.
“Nilipokuwa ndani, nimeshuhudia mengi na kweli siku hiyo polisi walikuwa wanahaha, kamanda wa polisi ametutembelea zaidi ya mara 3 kwa usiku huo” alisisitiza Lissu.
Lissu alilala mahabusu ya polisi baada ya kuhojiwa na kunyimwa dhamana ambapo siku moja alifikishwa mahakamani na kusomewa shitaka la uchochezi katika mahakama hiyo.
Kesi yake inasikilizwa na Hakimu Yohona Yongolo ambapo kwa upande wa mashitaka, unawakilishwa na Benard Kongolo, wakili wa serikali mkuu huku Lissu akitetewa na jopo la mawakili zaidi ya kumi wakiongozwa na Michael Ngalo akisaidiwa na Peter Kibatala
No comments:
Post a Comment