Mbunge wa
viti maalumu (CCM), Jackline Ngonyani jana alizua kizaazaa bungeni baada
ya kuwaambia wabunge wa upinzani wamekosa dira kiasi cha kula
rambirambi zilizotolewa kwenye msiba wa Philemon Ndesamburo.
Alitoa kauli
hiyo alipokuwa akichangia mjadala wa bajeti ya mwaka 2017/18. Baada ya
kuzungumzia hoja zake, Ngonyani alielezea kilichotokea kwenye salamu za
pole zilizotolewa wakati wa msiba wa muasisi huyo wa Chadema aliyewahi
pia kuwa mbunge wa Moshi Mjini kwa vipindi vitatu mfululizo.
Mbunge huyo
alianza kwa kumpongeza Rais John Magufuli kwa utekelezaji wa ilani ya
CCM na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo inawagusa wananchi,
akidai utekelezaji huo unawanyima hoja wapinzani.
Aliyafananisha
maneno ya wapinzani na miti kuteleza siku ya kifo cha nyani, akisema
licha ya kueleza kwamba Rais anatumia sera zao, wapinzani hao wamesahau
changamoto zinazowakabili wananchi kwenye majimbo yao.
Mbunge huyo alimshambulia mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari.
Alimshangaa
Heche kwa kuomba muongozo kutokana na wananchi wa jimbo lake kuvamia
mgodi wa North Mara ulio chini ya kampuni ya Acacia baada ya kukabiliana
na askari polisi.
Mwenyekiti
wa kikao hicho, Mussa Azzan Zungu alimtaka kuwasiliana na Waziri wa
Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kupata ufafanuzi wa suala hilo kutoka
serikalini.
“Huyu Heche
aliongea humu ndani kuhusu wananchi wake kulinda mgodi, leo anajikosha
kwa kuomba muongozo. Rais hakusema watu wakavamie migodi, hao wakamatwe
kama wahalifu wengine. Huyu naye akamatwe na kuunganishwa pamoja na
wavamizi hao,” alisema.
Baada ya
kauli hiyo, Heche alisimama na kumpa taarifa mbunge huyo kwa kueleza
kwamba jina lake linatumika vibaya. Alikumbusha kwamba wananchi wake
walifuatilia uwasilishaji wa ripoti ya kamati na kufahamu kwamba kampuni
hiyo ni feki.
“Nilisema sisi tumeumizwa, sasa kama unafikiri naogopa kuunganishwa hebu njoo unikamate wewe,” alisema.
Baada ya taarifa hiyo, Jackline alimwambia Heche: “Usinipotezee muda, nina mambo mengi ya kuzungumza.”
Baada ya
kuachana na Heche, mbunge huyo alimvaa Nasari kwa kueleza kwamba
alitumia dakika 10 alizopewa kulalamika juu ya uharibifu uliofanywa
kwenye shamba la maua la mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
“Hizi ni
akili au matope? Wananchi wake hawana changamoto? Ni mambo ya aibu
sana,” alisema mbunge huyo akikaribia kuhitimisha mchango wake kwenye
mjadala huo.
Kabla
hajakaa, sauti ilisikika ikimkumbusha suala la kuliwa kwa fedha za msiba
huo, kengele ya kuisha kwa muda wake ikiwa imeshagongwa, alitupa
kijembe wa upinzani.
“Nakushukuru sana mwenyekiti, naunga mkono hoja na (wapinzani) waache kula rambirambi za msiba wa Ndesamburo,” alisema Ngonyani.
Kauli hiyo iliwafanya wabunge wa upinzani wacharuke na kumtaka afute maneno hayo.
Alikuwa ni
mbunge wa viti maalumu (Chadema), Cecilia Pareso aliyemng’ang’ania baada
ya kutoa taarifa kwamba kilichozungumzwa na Jackline si sahihi na
kumtaka kufuta maneno hayo au kuthibitisha tuhuma hizo.
Mbunge huyo alikubali kuyaondoa maneno yake kwenye kumbukumbu kutokana na kukosa ushahidi wa alichokisema.
“Mwenyekiti,
kwa sababu ni suala la msiba, nayaondoa maneno hayo,” alisema na
kuhitimisha suala hilo lililowagusa wabunge wengi wa upinzani
waliokuwapo kwenye kikao cha jana asubuhi.
No comments:
Post a Comment